Muungano wa kijeshi Yemen wafanya mashambulio ya kisasi
8 Machi 2021Muungano huo ulifanya mashambulio hayo ya kulipiza kisasi baada ya msururu wa mashambulizi yaliofanywa na kundi hilo la waasi kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora yaliolenga ngome za kijeshi na taasisi za mafuta nchini Saudi Arabia.Muungano huo wa kijeshi pia umesema makombora yalilenga makazi ya raia nchini Saudi Arabia bila ya kutaja maeneo halisi. Msemaji wa muungano huo kanali Turki al- Maliki alinukuliwa na shirika rasmi la habari nchini Saudi Arabia akisema kuwa kulenga raia nataasisi zakiraia ni jambo lisilokubalika.
Wakazi katika mji wa Sanaa waliripoti kusikia milipuko mikubwa huku mabomu kadhaa yakianguka mjini humo japo idadi ya waathiriwa haikubainishwa mara moja. Kituo cha televisheni kinachomilikiwa na kundi hilo la waasi al- Masirah, kiliripoti kufanywa kwa mashambulizi saba ya angani katika wilaya za Attan na al-Nahda mjini Sanaa.
Huku mashambulio ya kundi hilo la waasi dhidi ya Saudi Arabia mara nyingi yakikosa kusababisha hasara ama kupatikana kwa waathiriwa, mashambulio dhidi ya taasisi kubwa za mafuta nchini humo yametatiza masoko ya nishati na uchumi wa dunia. Mashambulio hayo yameongezeka kwa masafa na usahihi katika wiki za hivi karibuni na kuibua wasiwasi kuhusu ulinzi wa angani wa Saudi Arabia na uwezekano wa kupanuka kwa kundi hilo la waasi nje ya mpaka wake.
Hii ni mara ya kwanza katika muda wa miezi kadhaa ambapo mji wa Sanaa umeshambuliwa na ndege za kivita za Saudi Arabia, tukio linalojiri wakati taifa hilo la kifalme linakabiliana na ongezeko kubwa la mashambulio katika mipaka yake dhidi ya miundo mbinu yake ikiwa ni pamoja na shambulio dhidi ya kituo kikubwa cha upakiaji mafuta katika Pwani yake hapo jana jioni. Wimbi hilo la mashambulio ya mabomu ya Saudia kwenye maeneo ya waasi wa Houthi ni la kwanza tangu tangazo lililosubiriwa kwa muda mrefu la Rais Joe Biden mwezi uliopita kwamba alikuwa anatamatisha msaada wa Marekani katika vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen, ikiwa ni pamoja na mauzo ya silaha kwa nchi hiyo.