1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa Merkel wapoteza jimbo muhimu

21 Januari 2013

Muungano wa vyama upinzani vya SPD na Kijani umetoa pigao kwa Kansela Angela Merkel kwa kushinda uchaguzi wa jimbo muhimu la Lower Saxony Jumapili, na kuimarisha matumaini yao katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba.

https://p.dw.com/p/17Nyk
Stephan Weil wa chama cha SPD akishangilia ushindi katika jimbo la Lower Saxony.
Stephan Weil wa chama cha SPD akishangilia ushindi katika jimbo la Lower Saxony.Picha: Reuters

Kiti kimoja kilibadilisha matokeo

Chama cha Kisoshial Democrat- SPD na mshirika wake chama cha Kijani vilishinda kwa kiti kimoja tu cha ubunge baada ya mchuano mkali katika jimbo hilo la nne kwa kuwa na wakaazi wengi nchini Ujerumani. Chama cha Kansela Merkel cha Christian Democratic Union CDU kiliyumba katika uchaguzi huu, lakini mshirika wake chama cha Free Democrats FDP kiliwashangaza waliyokitabiria kuondolewa kabisaa katika bunge la jimbo hilo mjini Hanover. Mgombea wa nafasi wa waziri mkuu kwa tiketi ya chama cha SPD Stephan Weil alisema ana uhakika wingi wa kura moja unaweza kutosheleza kabisaa.

Waziri mkuu aliyekuwa anatetea kiti chake, David McAllister wa chama cha CDU (kushoto) na mgombea wa SPD Stephan Weil (kulia).
Waziri mkuu aliyekuwa anatetea kiti chake, David McAllister wa chama cha CDU (kushoto) na mgombea wa SPD Stephan Weil (kulia).Picha: Getty Images

Kwa matokeo hayo, wadadisi wanasema Kansela Angela Merkel atalaazimika kupanua mkakati wake wa uchaguzi mkuu hapo Septemba. Mpinzani wa Merkel katika uchaguzi huo Peer Steinbrück alisema matokeo hayo yanaonyesha kuwa mchuano ndiyo kwanza unaanza. Merkel ambaye alitumia muda mwingi kumpigia kampeni mgombea wa chama chake David McAllister, waziri mkuu wa jimbo na ambaye anapewa nafasi ya kurithi nafasi yake, bado anaongoza katika uchunguzi wa maoni ya umma kutokana na namna alivyotetea maslahi ya Ujerumani katika mgogoro wa madeni wa Umoja wa Ulaya.

Wadadisi wanasema ushindi katika jimbo la Lower Saxony unaweza kuchochea kampeni za Steinbrück ambaye anakosea mara kwa mara. Baada ya mapigo kadhaa katika chaguzi za majimbo, chama cha Merkel cha CDU ndiyo kilipata kura nyingi zaidi kikiwa na asilimia 36. Washirika wake wa muongo mmoja FDP walipata karibu asilimia 10, na kuvuka makadirio ya waendesha kura za maoni waliyokitabiria chama hicho kuanguka kabisaa.

Wafuasi wa mgombea wa chama cha kijani wakishangilia matokeo.
Wafuasi wa mgombea wa chama cha kijani wakishangilia matokeo.Picha: Getty Images

Ni gharama ya CDU kutaka kumbeba mshirika wake FDP

Lakini matokeo yao ya jumla yalikuwa chini ya muungano wa SPD waliopata asilimia 33 na kijani waliyopata asilimia 14, hii ikimaanisha kuwa upinzani sasa unaweza kuunda serikali ya jimbo hilo. Chama cha FDP kilinufaika kutokana na wapiga kura wa chama Merkel waliogawanya kura zao chini ya mfumo wa kura mbili kujaribu kunusuru muungano. Karibu wapiga kura 101,000 waliyoipigia CDU mwaka 2008 waliipigia FDP siku ya Jumapili.

Wapiga kura milioni 6.2 waliandikishwa katika uchaguzi wa jimbo hilo la kaskazini magharibi, ambalo ndiyo nyumbani kwa kampuni kubwa ya magari ya Volkswagen. Kama FDP ingeshindwa kupata uwakilishi, mwenyekiti wake Philip Roesler ambaye ndiye naibu wa Merkel katika serikali na waziri wa uchumi na ambaye anatokea katika jimbo la Lower Saxony angekabiliwa na shinikizo la kujiuzulu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFPE, RTRE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir