1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvua ya mabao Allianz Arena

17 Oktoba 2022

Serge Gnabry, Leroy Sane, Sadio Mane, Eric Maxim Choupo Moting na Marcel Sabitzer ndio wachezaji watano wa Bayern Munich walioifungia timu yao Jumapili walipokuwa wakicheza na SC Freiburg.

https://p.dw.com/p/4II9F
Bayern München - SC Freiburg
Picha: Matthias Schrader/AP/picture alliance

Bayern walivuna ushindi wa magoli 5-0 katika uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena katika mpambano wa Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga.

Kwa ushindi huo Bayern sasa wanaishikilia nafasi ya pili katika msimamo wa Bundesliga wakiwa na pointi 19 pointi nne nyuma ya vinara Union Berlin ambao hiyo Jumapili pia walipata ushindi wa rahisi wa 2-0 walipokuwa wakikwaana na Borussia Dortmund.

Janik Haberer ndiye aliyekuwa mfungaji wa mabao yote mawili ya Union katika mechi ambayo Dortmund ilishuhudia kurudi kikosini kwa nahodha wao Marco reus aliyekuwa nje kwa mechi kadhaa kutokana na jeraha.

Orodha ya wafungaji bora inaongozwa na Niclas Fulkrüg mshambuliaji wa Werder Bremen aliye na jumla ya magoli 8 kufikia sasa naye Marcus Thuram na Christopher Nkunku wanamfuata wakiwa na mabao 7 kila mmoja.

Daichi Kamada na Sheraldo Beckker wana mabao 6 kila mmoja kisha orodha ya wenye mabao 5 inatawalwa na wachezaji wa Bayern Sadio Mane, Leroy Sane na Jamal Musiala kisha Dodi Lukebakio ndiye mwengine aliye kwenye orodha hiyo.