1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya matajiri na masikini katika mikakati ya kupambana na ujoto duniani baada ya 2012.

Mohammed AbdulRahman17 Novemba 2006

Watetezi wa Kyoto wasema hakuna mbadala isipoku nchi ziwajibike ili kuepukana na kitisho kikubwa cha maisha duniani.

https://p.dw.com/p/CHm8
Nembo ya mkutano wa kimataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Nembo ya mkutano wa kimataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Mataifa tajiri na masikini yamejikuta yakivutana juu ya njia za kutanua hatua za kupambana na ujoto duniani baada ya 2012, ili kuyaokoa mazungumzo ya Umoja wa mataifa kuhusu kukabiliana na kile wajumbe wengi wanachokiita, moja kati ya vitisho vikubwa vya maisha duniani.

Kiasi ya mawaziri 70 wa mazingira wanaohudhuria mkutano huo wa Nairobi, wamekubaliana juu ya hatua za kulisaidia bara la Afrika na mataifa mengine masikini, yaweze kukabiliana na athari zinazohofiwa za majanga kama mafuriko na ukame. Lakini wamegawika mno kuhusiana na jinsi ya kuutanua waraka wa Kyoto unaolenga kupunguza ongezeko la ujoto duniani.

Waziri wa mazingira wa Ujerumani Bibi Sigmar Gabriel alisema “ baadhi ya wakati si rahisi kuyatatua matatizo miongoni mwa pande mbili ziliomo serikalini nchini Ujerumani na hapa kuna mataifa 189 na ni vigumu kupata maafikiano.”

Katika mkutano huo wa mazingira, mengi miongoni mwa mataifa tajiri yanashikilia kupitiwa kwa undani waraka wa Kyoto, ambao unaweka viwango vya utoaji gesi zinazoharibu mazingira kutoka mataifa 35 yalioendelea kiviwanda, kabla ya kuchukua hatua kali zaidi baada ya 2012, wakati muda wa utekelezaji wa viwango vya sasa utakapomalizika.

Baadhi ya mataifa masikini yanahofia kupitiawa kwa undani waraka huo wa Kyoto inaweza kuwa ni njia ya kuyaingiza mataiafa hayo katika gharama kubwa.Taarifa ya mataifa ya Kiafrika ilisema kwa kiasi wanachohusika wao, ni kwamba kupitiwa kwa Kyoto kulikopangwa kwa ajili ya mkutano wa Nairobi chini ya yaliomo katika makubaliano ya 1997, kumeshafanyika.

Mataifa masikini yanasema nchi tajiri hazina budi sasa kuzingatia uwekaji wa hatua kali zaidi baada ya 2012, kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira na kusababisha ongezeko la joto, hasa kutokana na moshi wa viwanda na magari.

Marekani chini ya utawala wa Rais Bush ni moja wapo ya nchi zilizokataa kutekeleza waraka huo , ikisema utahujumu uchumi wake. Jeremy Symons mmoja wa wanaharakati wa kampeni ya kupambana na ongezeko la ujoto duniani nchini Marekani, akizungumzia hali hiyo anasema,“Zingatio letu sasa ni kuhakikisha Marekani inapunguza utoaji gesi zinazosababisha ongezeko la joto haraka iwezekanavyo.Tunaelekea njia mbaya.”

Kwa upande mwengine Umoja wa Ulaya ambao unatoa asili mia 14 ya hewa chafu duniani, unataka nchi masikini zianze kupunguza utoaji wa gesi za aina hiyo upande wao, lakini Waziri wa mazingira wa Finland Jan Erik Enestam alisema umoja wa Ulaya hautaki paweko na vifungu vipya katika waraka wa Kyoto kwa ajili ya mataifa yanayoendelea.

Mbunge wa chama cha kijani katika bunge la Ujerumani Bundestag Reinhard Loske anayehudhuria mkutano huo wa mazingira, ametahadharisha juu ya kuzuka kambi mbili katika suala hilo la utekelezaji wa waraka wa Kyoto- ikiwa ni kati ya wapinzani ambao ni nchi za viwanda vinavyotegemea mafuta kama Marekani na zile zinazotaka kutekelezwa waraka huo zikisema hali haiwezi kuendelea kama ilivyo.

Bw Loske akasema yote hayo hayana budi kuwekwa wazi mjini Nairobi, lakini kwa hakika hakuna mbadala isipokua tu kutekelezwa kwa makubaliano ya Kyoto. Mkutano huo wa mazingira juu ya hali ya ujoto duniani mjini Nairobi unamalizika leo.