Mvutano waibuka Umoja wa Mataifa juu ya ziara ya Al-Aqsa
6 Januari 2023Mabalozi wa Israel na Palestina katika Umoja wa Mataifa jana walirushiana maneno makali katika Baraza la Usalama la Umoja huo kuhusu ziara yenye utata ya Waziri wa Usalama wa Israel, Itamar Ben-Gvir, kwenye eneo la msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem.
Balozi wa Israel, Gilad Erdan, amekiita kikao hicho cha "kipuuzi", huku Balozi wa Palestina, Riyad Mansour, akilishutumu taifa hilo la Kiyahudi kwa kufanya kitendo cha dharau.
Mkutano wa kuijadili ziara hiyo umefanyika kutokana na ombi la Umoja wa Falme za Kiarabu na China.
Erdan alisema hakuna sababu ya mkutano huo kufanyika. Ziara ya Ben-Gvir siku ya Jumanne, imezusha ukosoaji mkali wa kimataifa, ikiwemo kutoka kwa Marekani, mshirika wa muda mrefu wa Israel.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake na kusisitiza umuhimu wa kudumisha hali iliyopo sasa katika eneo hilo la msikiti.