1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa nchini Ethiopia

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
6 Novemba 2020

Mgogoro wa nchini Ethiopia kati ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na serikali kuu ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia umeongeza mivutano katika taifa hilo lenye tofauti za kikabila.

https://p.dw.com/p/3kxrb
Norwegen l Verleihung des Friedensnobelpreis an Abiy Ahmed in Oslo
Picha: picture alliance/AP Photo/NTB scanpix/H. M. Larsen

Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliyemwagiwa sifa maridhawa pale aliposhinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka jana sasa anakabiliwa na mtihani mkubwa tangu alipoingia madarakani na kuanza kuleta mageuzi haswa huko Tigray ambako mzozo wa silaha unatishia utulivu katika nchi ya pili yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema operesheni za kijeshi zinazofanyika katika mkoa wa kaskazini wa Tigray zina malengo maalum wakati ambapo miito inaongezeka kwa nchi hiyo kujiepusha na kile kinachowezakusababaisha vita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitaka pande zote zinazohusika kujiepusha na mzozo huo mara moja huku kukiwa na ripoti za kutumika silaha kuongezeka na harakati za kijeshi. Waangalizi wametahadharisha kuwa vita kati ya majeshi mawili yenye nguvu vinaweza kuwa vya muda mrefu na pia vitasababisha umwagikaji damu.

Kiongozi wa jimbo la Tigray Dr. Debretsion Gebremichael
Kiongozi wa jimbo la Tigray Dr. Debretsion GebremichaelPicha: DW/M. Haileselassie

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wya Ethiopia Dina Mufti amesema serikali imewaambia wanadiplomasia kwamba ilichokozwa hatua iliyosababisha hali iliyopo sasa. Lakini inataka amani na utulivu nchini Ethiopia na inataka suala hili litatuliwe haraka.

Kwa upande wake kiongozi wa Tigray Debretsion Gebremichael amesema mapigano yaliendelea kwenye eneo la magharibi mwa Tigray, na kwamba wanajeshi wa serikali wanakusanyika mpakani katika mikoa jirani ya Amhara na Afar. Amesema wana nguvu na vifaa vya kutosha vya kijeshi kukabiliana na uvamizi kutoka nje.

Wasiwasi wa kutokea vita unatokana na uhasama wa muda mrefu kati ya serikali ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF), ambacho maafisa wake wanalalamika kuwa wametengwa chini ya utawala wa waziri mkuu huyo na wanamlaumu Abiy Ahmed kwa kuchochea vita na kutoamadai yasiyokuwa ya kweli ili kuhalalisha uvamizi dhidi ya jimbo la Tigray.

Chanzo: AFP/RTRE