1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

240209 Kuba Machtwechsel

Charo, Josephat/ Castritius, Michael24 Februari 2009

Hali bado ni kama ilivyokuwa zamani chini ya utawala wa kakake Fidel Castro

https://p.dw.com/p/H0J0
Rais wa Cuba Raul CastroPicha: AP

Februari 24 mwaka 2008 Raul Castro alichaguliwa na bunge la Cuba kuwa rais mpya wa nchi hiyo. Hatua hiyo ilimaliza utawala wa miaka 49 wa kakake Fidel Castro. Raul Castro aliwekewa matumaini makubwa ya kufanya mageuzi hususan katika swala la utumiaji wa bidhaa, lakini kufikia majira ya kiangazi matumaini hayo yalikuwa tayari yamekufa. Hakukuwa na upenyo wowote nchini Cuba, huku taifa hilo likinyamaa kimya kwenye ukumbi mkubwa wa kusubiri katika historia yake.

Katika mji mkuu wa Cuba, Havanna, kila kitu kinabakia kama zamani. Kama ilivyokuwa wakati wa Fidel Castro ndivyo iliyvyo wakati huu wa utawala wa kakake Raul Castro. Kwa sababu kufikia sasa Raul mwenye umri wa miaka 77 hajafaulu kufanya mageuzi ya maana. Wacuba wanalazimika kusubiri kwenye foleni ndefu madukani, katika ofisi za serikali na kwenye barabara za nchi hiyo ambazo zinakaribia kuwa bila magari. Wanasubiri kuboreka kwa hali yao ya maisha. Rais Raul Castro mwenyewe alizusha matumaini makubwa kwamba angechukua hatua za kwanza, kwa mfano katika hotuba yake mwaka mmoja uliopita.

"Bila upendeleo kuna vikwazo. Tunavijua na tunalazimika kuteseka chini ya vikwazo hivyo kila siku. Tuna idadi kubwa ya marufuku na sheria zinazovuka mpaka. Tunaanza kuzipiga marufuku sheria zile rahisi. Sheria nyingine zinahitaji muda zaidi. Uchunguzi lazima ufanywe kwanza na sheria zibadilishwe. Lazima tuboreshe utendaji kazi wa serikali yetu."

Lakini matumaini hayo yalidumu msimu mmoja tu wa machipuko. Mwezi Aprili na Mei mwaka 2008 mageuzi machache yalifanyika, ambayo yaliathiri sekta ya utumiaji wa bidhaa. Vitu kama kompyuta, vifaa cha kuchezea DVD, vifaa cha kupikia mchele au baiskeli yenye kifaa cha umeme vilianza kununuliwa kwa uhuru wakati huo. Wacuba waliruhusiwa kulala katika hoteli zote nchini Cuba na ilikuwa halali kumiliki simu za mkono. Hatua hizi mpya zilitoa sura mpya ya Cuba hususan katika nchi za kigeni, anasema Richard Haep, anayefanyakazi na shirika la misaada la Ujerumani, Deutsche Hungerhilfe, nchini Cuba.

"Mageuzi haya yalikuwa ya kwanza na yameidhinisha tu kile ambacho tayari kimekuwa kikifanyika kwa muda mrefu. Kila raia wa Cuba aliyetaka na aliyeweza kulipa, alikuwa pia na simu ya mkono. Alimuuliza raia yeyote wa kigeni kama alitaka kumfanyia mkataba. Hiyo ni mojawapo ya marufuku za kipuuzi ambazo rais Raul Castro alizitaja katika hotuba yake. Hilo bila shaka ni jambo ambalo jumuiya ya kimataifa inalitambua lakini hapa nchini kwa kweli halina maana yoyote."

Juu ya hayo, uhuru huu wa utumiaji wa bidhaa ulibanwa kwa sababu bidhaa ziliuzwa kwa sarafu ya CUC (kuk) badala ya sarafu ya Cuba ya Peso. Sarafu ya CUC ni sarafu ya siri inayochukua nafasi ya dola, ambayo kutumia hiyo mtu anaweza kuishi vizuri katika kisiwa cha Cuba. Hupatikana kutoka kwa jamaa wanaoishi nchi za kigeni au kupitia kazi kwenye sekta ya utalii.

Raia wanyonge wasioweza kuipata sarafu hii hawawezi kunufaika kutokana na uhuru wa utumiaji wa bidhaa. Miongoni mwao ni Carlos, kijana wa miaka 26, anayefanyakazi kama bawabu kwenye afisi moja ya serikali. Anapokea Peso 480, kwa mwezi, ikiwa ni sawa na yuro 16. Kwa pesa hizi anaweza tu kugharimia mchele, maharagwe na pombe kali ya bei rahisi. Chini ya utawala wa Raul Castro hakuna kilichobadilika, anasema Carlos anayeishi kwenye kitongoji cha watu maskini cha Alamar mjini Havanna.

"Kitu pekee kilichobadilika ni usafiri wa mwendo mfupi ambao umeboreka kidogo. Mishahara nayo imeongezeka. Ni wazi kwamba sasa tunaweza kununua kompyuta, lakini inagharimu CUC 800.(inatamkwa kuk) Nitazitoa wapi pesa hizo huku mshahara wangu ni CUC 20 tu kwa mwezi? Hiyo ni hadaa, serikali inatuhadaa. Juu ya hayo kila kitu kimefungwa hapa, hatuwezi kusafiri hata kwenda nchi maskini sana ya Haiti. Kilichosalia kwetu ni kuingia kwenye dau na kujaribu kwenda Miami. Nakueleza haya bila uoga lakini polisi akinisikia nitakamatwa. Hakuna uhuru wa vyombo vya habari hapa."

Tangu majira ya kiangazi hakujakuwa na mageuzi mengine. Vimbunga vitatu vilipiga Cuba na kusababisha hasara ya yuro bilioni saba. Rais Fidel Castro alitoa maneno makali yaliyomzima kakake Raul.

Raul amefaulu tu katika ngazi ya kimataifa kwa kuufanya upya uhusiano na Urusi na kumkaribisha rais wa China mjini Havanna. Viongozi wa serikali za Amerika Kusini wamemkumbatia Raul pamoja na Cuba nzima na wanaitaka Marekani iondoe vikwazo dhidi ya kisiwa hicho. Matumaini ya Wacuba wengi hayatafikiwa kupitia rais mpya wa Marekani Barak Obama chini ya utawala wa akina Castro.