1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanafunzi awauwa takribani watu 14 kwa risasi Prague

22 Desemba 2023

Mwanafunzi alifyatua risasi jana katika chuo kikuu kimoja cha mji mkuu wa Jamhuri ya Czech, Prague na kuwauwa karibu watu 14 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 20.

https://p.dw.com/p/4aSwk
Tschechien Prag 2023 | Schusswaffenangriff an Karls-Universität
Picha: Michal Cizek/AFP/Getty Images

Hilo ndio tukio baya kabisa la ufyatuaji risasi dhidi ya watu wengi kuwahi kushuhudiwa katika nchi hiyo. Mkuu wa Polisi ya Prague Martin Vondrasek amesema umwagaji damu huo ulitokea katika jengo la idara ya filosofia la Chuo Kikuu cha Charles, ambako mshambuliaji huyo alikuwa ni mwanafunzi. Maafisa wameonya kuwa idadi ya vifo huenda ikapanda. Polisi hawakutoa maelezo kuhusu waathirika au chanzo cha shambulizi hilo. Awali, polisi waliwaambia wakazi kuepuka eneo hilo na kubaki majumbani wakisema operesheni zao zinaendelea. Dakika chache baadae wakasema mshambuliaji huyo ameuawa. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Czech Vit Rakusan alisema wapelelezi hawashuku kuwa kuna uhusiano na itikadi kali au vikundi vyovyote vya itikadi kali. Vondrasek amesema polisi wanaamini mshukiwa huyo alimuuwa babake mapema jana katika mji wake wa kuzaliwa Hostoun, magharibi mwa Prague, na kuwa alikuwa akipanga pia kujiuwa.