1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarungi asema yuko salama baada ya kutekwa Nairobi

Sylvia Mwehozi
13 Januari 2025

Mwanaharakati wa haki za binaadamu nchini Tanzania Maria Sarungi Tsehai amesema yuko salama baada ya kuripotiwa kutekwa nyara katika mitaa ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi siku ya Jumapili (12.01.2025).

https://p.dw.com/p/4p50Q
Mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai
Mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi TsehaiPicha: Imani Nsamila

Taarifa iliyotolewa na shirika la Amnesty International na kusambaa siku ya Jumapili, ilisema kuwa mwanaharakati huyo mashuhuri wa haki za binaadamu nchini Tanzania Maria Sarungi Tsehai alitekwa nyara katika mitaa ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi siku ya Jumapili (12.01.2025).

Muda mchache baadae, Maria Sarungi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, aliandika kwamba "Mungu ni mwema! Nimepambana na ninyi mmepambana. Niko salama, shukrani kwa kila mmoja na nitazungumza kesho".

Soma: Kada wa upinzani apatikana na majeraha baada ya 'kutekwa'

Tsehai amekuwa akifanya kampeni za kuwepo mabadiliko ya kisiasa, uhuru wa kujieleza na kutetea haki za wanawake nchini Tanzania na ana wafuasi milioni 1.3 kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Awali Shirika la Amnesty International tawi la Kenya lilisema kuwa Tsehai "alitekwa nyara na watu watatu waliokuwa na silaha na kupakiwa kwenye gari nyeusi aina ya Toyota Noah" majira ya saa tisa alasiri katika eneo la Kilimani katikati mwa Nairobi.

Sarungi Tsehai
Maria Sarungi TsehaiPicha: Imani Nsamila

Nalo shirika lake la Change Tanzania, limeandika kwenye mtandao wa X kwamba; "Tunaamini waliomteka nyara ni sehemu ya maafisa wa usalama wa Tanzania wanaofanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania ili kunyamazisha ukosoaji halali." Shirika hilo limeongeza kuwa "ujasiri wake wa kutetea haki umemfanya kuwa mlengwa, lakini hatutaruhusu wakati huu kunyamazisha sauti yake."

Soma: Rais wa Kenya aahidi kukomesha utekaji nyara

Kenya imekuwa na historia ya kuruhusu serikali za kigeni kuwateka nyara raia wao na kuwarudisha kwa lazima kinyume na sheria za kimataifa.

Mnamo mwezi Oktoba, Umoja wa Mataifa ulielezea "wasiwasi mkubwa" juu ya ripoti kwamba wakimbizi wanne wa Kituruki walitekwa nyara jijini Nairobi na kurudishwa Uturuki kwa lazima.

Mwezi uliofuata, Uganda ilisema kuwa ilishirikiana na mamlaka za Kenya kumkamata kiongozi wa upinzani wa Uganda, Kizza Besigye, mjini Nairobi na kumrejesha nyumbani ambako anakabiliwa na kesi inayokosolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Amnesty International ilionya kuwa ni sehemu ya "mwenendo unaozidi kushamiri na unaotia wasiwasi wa ukandamizaji wa kimataifa" nchini Kenya.

Chanzo: (AFP)