Mwandishi habari wa Ujerumani Deniz Yücel aachiwa huru!
16 Februari 2018Serikali ya Ujerumani imefurahishwa juu ya habari hizo za kuachiwa huru kwa mwandishi habari huyo wa gazeti la Ujerumani la Die Welt. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel alipitisha juhudi kubwa mnamo siku za hivi karibuni kwa ajili ya mwandishi huyo.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amesisitiza kwamba hapakuwapo makubaliano yoyote ya pembeni juu ya kuachiwa kwa mwandishi huyo Hata hivyo mwanasiasa wa chama cha mrengo wa shoto Dagdelen anatuhumu kwamba isingeliwezekana kwa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kumwachia mwandishi huyo bila ya kupata chochote kutoka Ujerumani.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema amefurahi sana juu ya uamuzi wa mahakama ya nchini Uturuki wa kumwachia huru mwandishi huyo wa gazeti la Die Welt. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel naye amesema amefurahishwa kutolewa jela kwa mwandishi wa habari wa Ujerumani mwenye asili ya Kituruki Deniz Yucel na ameitolea mwito Uturuki ihakikishe kuwa kesi zinayowakabili wananchi wengine wa Ujerumani zisikilizwe kwa haraka.
Vyombo vya habari vya serikali nchini Uturuki vimethibitisha kwamba bwana Yücel ameachiwa kwa dhamana baada ya kuwekwa mahabusu. Mwandshi huyo aliwekwa ndani kwa muda wa mwaka mmoja bila ya kufunguliwa mashtaka kadhia iliyosababisha uhusiano baina ya Ujerumani na Uturuki ukwaruzike.Waendesha mashtaka wa Uturuki wanatuhumu kwamba bwana Yücel anahusika na kuendesha propaganda ya kigaidi na kuchochea chuki na uadui katika jamii.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alimwambia waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim hapo jana kwamba kuwekwa mahabusu kwa mwandishi Yücel kilikuwa ni kizingiti kirefu katika uhusiano baina ya Ujerumani na Uturuki. Merkel alimwambia waziri mkuu huyo wa Uturuki aliyefanya ziara nchini Ujerumani kwamba nchi zao mbili zina maslahi ya pamoja katika dhamira ya kuboresha uhusiano baina yao, katika msingi wa maadili ya pamoja.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildirim amesema, Baadhi ya tofauti kati ya Uturuki na Ujerumani zimetatuliwa, aliyasema hayo muda mchache baada ya mahakama nchini mwake kuamuru kuachiwa huru kwa mwandishi huyo wa habari wa Ujerumani mwenye nasaba ya Kituruki Deniz Yucel. Waziri huyo mkuu wa Uturuki ambaye yuko mjini Munich kuhudhuria mkutano wa masuala ya usalama amesema pande zote mbili akimaanisha Uturuki na Ujerumani zitashirikiana kuuboresha uhusiano baina yao.
Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas naye ameandika kupitia kwenye mtandao waTwitter kwamba kufunguliwa kwa bwana Yücel ni habari nzuri kabisa kuwahi kusikika katika kipindi cha muda mrefu uliopita. Mke wa Yucel, Bi Dilek Mayaturk-Yucel, aliandika pia ujumbe wa Twitter uliosema "Hatimaye !!! Deniz yuko huru! ". Bi Yucel amesema kwa hakika amefurahi kwa niaba yake na ya mume wake pamoja na familia kwa jumla.
Mwandishi:Zainab Aziz/DPAE
Mhariri:Yusuf Saumu