Mwandishi wa El-Salvador atunukiwa Tuzo ya DW 2023
4 Mei 2023Shirika la Utangazaji la kimataifa la Ujerumani, DW limemtangaza mwandishi habari Oscar Martinez kuwa mshindi wa tuzo yake ya mwaka huu, ikitambua mchango mkubwa uliotolewa na mwandishi huyo kutoka El Salvador katika kuzikabili shinikizo zinazowaandama waandishi habari nchini mwake.
Martinez mwenye umri wa miaka 40 ni mhariri mkuu wa gazeti la mtandaoni nchini El-Salvador linaloitwa El Faro ambalo lilianzishwa mnamo mwaka 1998 likiwa kama mradi uliokuwa hauna bajeti na baadae likageuka kuwa moja ya chombo cha habari maarufu kinachoongoza katika habari za uchunguzi katika kanda ya Amerika ya Kusini.
Tuzo ya Dw ya uhuru wa habari ya mwaka huu imetangazwa leo Mei 3 ikiwa pia ni siku ya kumbukumbu ya miaka 70tangu kuanzishwa kwa shirika hili la habari la Umma la Ujerumani, DW.
Mkuu wa DW asema Martinez ameonesha kuwa jasiri licha ya vikwazo
Mkurugenzi mkuu mtendaji wa DW Peter Limbourg ameeleza tuzo hiyo imetolewa kwa Martinez kwa sababu ''Oscar Martinez ni mwandishi habari jasiri ambaye anapigania uhuru wa vyombo vya habari na maoni, na kupitia gazeti lake na kituo chake ni mfano ambaye bila shaka kwa watazamaji,na wasomaji wa makala zake ambaye anapigania maslahi yao na jasiri.''
Katika suala zima la kupigania uhuru wa habari Oscar Martinez na wafanyakazi wote wa gazeti la El Faro wanasimama kupambana na shinikizo kubwa wanalolipata waandishi habari nchini ElSalvador pamoja na kwenye nchi nyingine za Amerika ya kati katika kazi zao,
''Nafikiri changamoto zinazowakabili waandishi hivi sasa ni kubwa kwasababu kuna nguvu kubwa zinazopambana na waandishi habari zinazojaribu kuwazuia kufanya kazi zao na kwahivyo nafikiri hali inazidi kuwa ngumu kwao na hasa kutokana na kuwepo kampeini za kuwachafua na chuki dhidi ya waandishi na uandishi,kukiweko hatari ya kushambuliwa kuanzia mitandaoni lakini mpaka mashambulizi ya kimwili.Na hali hii inashuhudiwa kote ulimwenguni.'' amesema mkurugenzi mkuu huyo wa Dw Peter Limbourg.
Juhudi za Martinez ndiyo chanzo cha kupatiwa tuzo ya DW 2023
Tuzo ya uhuru wa habari ya Dw imetunukiwa Oscar Martinez kutokana na juhudi zake pamoja na ujasiri wa kutowa habari zisizokuwa na upendeleo kwa wasomaji wake kwa kuhatarisha maisha yake.
Martinez anasema;
"Tunaamini uandishi unapaswa kufanya mambo muhimu mawili,kusimamia madaraka na wenye madaraka. Kuonesha dosari za madaraka na mifumo yake. Na la pili ni kuonesha maisha ya walio wanyonge kabisa kutokana na athari za wale wenye madaraka makubwa.Na tunaamini kwamba yote haya yanaonekana hivi sasa ambapo kanda nzima ya Amerika ya kati inakabiliwa na wimbi jipya la uimla."
Nchini El-Salvador haki za kikatiba kwa mfano uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kukusanyika ni mambo yaliyopigwa marufuku tangu serikali ya nchi hiyo ilipotangaza amri ya hali ya hatari mnamo mwezi March mwaka jana.
Tuzo ya uhuru wa utoaji habari ya DW Fosa imekuwa ikitolewa tangu mwaka 2015 ikitunukiwa kwa waandishi walionesha juhudi za kuunga mkono haki ya kuwepo uhuru na hasa uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa vyombo vya habari.