Mwelekeo wa deni la taifa Kenya ni "mbaya"
9 Julai 2024Hii ikimaanisha kwamba nchi hiyo ya Afrika mashariki italilipa deni lake kwa kiwango cha juu zaidi cha riba.
Moody's imetahadharisha kuwa hali si nzuri kwa nchi hiyo kufuatia wimbi la maandamano yaliyoipelekea serikali kutupilia mbali mapendekezo ya nyongeza ya kodi.
Rais William Ruto, anakabiliwa na mzozo mkubwa zaidi katika hatamu ya urais wake wa karibu miaka miwili, mwezi uliopita alitupilia mbali mswada wa fedha uliolenga kujaza hazina ya serikali na kusaidia kupunguza mzigo wake mkubwa wa deni.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana wa Kenya maarufu kama Gen-Z kupinga nyongeza ya ushuru ambayo ilitishia kuongeza ugumu wa kiuchumi wa watu ambao tayari wanakabiliwa na gharama ya juu ya maisha.
Soma pia: Hazina: Deni la Kenya lapanda hadi kiwango cha kihistoria
Shirika hilo la uorodheshaji wa madeni lenye makao yake makuu nchini Marekani, katika taarifa yake limesema linaishusha Kenya kwa ngazi moja zaidi hadi Caa1 kiwango kinachozingatiwa kuwa na "hatari kubwa sana kwa mkopo".
Makadirio haya mapya ya shirika la Moody's, na mtazamo wake hasi kwa nchi taifa hilo la Afrika Mashariki, huenda ukaongeza zaidi gharama za kukopa kwa serikali inayokabiliwa na matatizo ya kifedha.
Shirika la Moody's limesema kushushwa kwa kiwango hicho kunaonyesha "uwezo uliopungua" wa Kenya wa kuongeza kodi na kupunguza deni lake.
"Hasa, uamuzi wa serikali wa kutofuata nyongeza ya kodi iliyopangwa na badala yake kutegemea kupunguzwa kwa matumizi ili kupunguza nakisi ya kifedha inawakilisha mabadiliko makubwa ya sera na athari za nyenzo kwa mwelekeo wa kifedha wa Kenya na mahitaji ya kifedha," ilisema.
"Katika muktadha wa mvutano mkubwa wa kijamii, hatutarajii serikali kuwa na uwezo wa kuanzisha hatua muhimu za kuongeza mapato katika siku zijazo."
Gharama ya maisha
Rais Ruto alitangaza mnamo Juni 26 kwamba anauondoa mswada wa fedha ambao ulilenga kukusanya zaidi ya dola bilioni 2.7 baada ya maandamano ya amani juu ya kupinga nyongeza ya kodi kugeuka na kuwa machafuko.
Kulingana na tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu, takriban watu 39 wameuawa tangu maandamano yalipoanza Juni 18, huku hasira ya ongezeko la kodi likibadili shinikizo lake na kuwa kampeni inayoendelea dhidi ya Ruto na serikali yake.
Soma pia: Bajeti kuu Kenya yagonga sh. 3.3 Trilion
Ijumaa iliyopita, Ruto alisema serikali ililazimika kufidia ukosefu wa mapato ya ziada ya ushuru, akitangaza kupunguzwa kwa bajeti ya shilingi bilioni 177 (dola bilioni 1.4) na kukopa zaidi kwa karibu shilingi bilioni 169.
Deni la taifa lazidi kupanda
Deni la taifa la Kenya tayari linafikia takriban shilingi trilioni 10, karibu asilimia 70 ya pato jumla la taifa.
Licha ya msukosuko huo, shilingi ya Kenya kwa kiasi kikubwa imeendelea kuwa madhubuti kwa sasa ikiwa dola moja inabadilishwa kwa shilingi 128, baada ya kudorora na kufikia shilingi 160 kwa dola moja ya Marekani mnamo mwezi Januari.
Mamlaka ya Mapato nchini Kenya, KRA, ilitangaza kwamba ilikuwa imekusanya shilingi trilioni 2.4 katika mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 30, hilo likiwa ongezeko la zaidi ya asilimia 11, lakini asilimia 4.5 chini ya lengo.