1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yasema tayari inawalinda Warohingya

24 Januari 2020

Serikali ya Myanmar ilishaweka mfumo madhubuti wa hatua za kuwalinda Waislamu wa jamii ya Rohingya, siku moja baada ya mahakama ya haki ya Kimatraifa kuitaka ifanye hivyo haraka

https://p.dw.com/p/3Wm2Z
Niederlande Justiz l Protest gegen die Führer Myanmars vor dem Internationalen Gerichtshof in Den Haag
Picha: DW/A. Islam

Siku moja baada ya Mahakama ya Haki ya Kimataifa kuiamuru Myanmar kuchukuwa hatua za haraka na makusudi kukomesha vitendo vya mauaji ya halaiki dhidi ya jamii ya Waislamu wa Rohingya, kufuatia kesi iliyofunguliwa na Gambia, serikali ya Myanmar imepuuzilia mbali amri hiyo ikisema ilishaweka mfumo madhubuti wa hatua za kuwalinda Waislamu hao zamani. 

Msemaji wa chama tawala cha National League for Democracy, Myo Nyunt, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa serikali tayari inayatekeleza maagizo hayo yaliyotolewa na Mahakama ya Haki ya Kimataifa - ICJ. Amesema kitu kimoja ambacho Myanmar inapaswa kufanya ni kutoa ripoti, akimaanisha mojawapo ya hatua zilizoidhinishwa na mahakama ikiitaka Myanmar kuandika ripoti za mara kwa mara za hatua inazopiga.

Niederlande Den Haag Völkermordklage gegen Myanmar
Mahakama ya Haki ya Kimataifa mjini The HaguePicha: picture alliance/dpa/AP/P. Dejong

Lakini amesema serikali ya kiraia, ambayo inaongoza kwa pamoja na jeshi katika mpangilio mgumu wa kikatiba ambao unampa madaraka mengi amiri jeshi mkuu, haiwezi kuwadhibiti wanajeshi.

Amesema kuwa chini ya mazingira ya sasa ya kisiasa, wana matatizo ya kutatua baadhi ya masuala – kama vile amri kuwa serikali lazima ihakikishe jeshi lake au wanamgambo wenye silaha hawafanya vitendo vya mauaji ya halaiki au kujaribu kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Warohingya au Wabengali.

Zaidi ya Warohingya 730,000 walikimbia jimbo la magharibi la Rakhine na kuhamia nchi jirani Bangladesh mwaka wa 2017 ili kuepuka ukandamazaji ambao Umoja wa Mataifa ulisema ulifanywa kwa nia ya mauaji ya kimbari. Myanmar inasema operesheni hiyo ya kijeshi ilikuwa halali kwa ajili kupambana na uasi iliyoanzishwa kuyajibu mashambulizi ya wanamgambo wa itikadi kali dhidi ya vikosi vya usalama.

Myanmar Rohingya-Flüchtlinge aus Bangladesch | Polizei & Journalisten Thet Kae Pyin-Camp
Polisi wakiwa katka kambi ya Warohingya ya Thet Kae PyinPicha: Getty Images/AFP/P. Hein Kyaw

Mahakama ya ICJ yenye makao yake mjini The Hague ilisema katika hukumu yake jana kuwa haikubali tamko la Myanmar kuwa imekuwa ikichukua hatua za kusaidia kurejea nyumbani kwa wakimbizi, kuhimiza amani katika jimbo la Rakhine, na kuliwajibisha jeshi kupitia mifumo ya ndani ya nchi.

Wakati uamuzi huo wa mahakama ulikuwa ushindi wa kihisia kwa watu wa jamii hiyo ya walio wachache, ambao kwa miongo mingi wamepambana kuthibitisha uwepo wao kama jamii, wachambuzi wa kisheria wanasema itakuwa vigumu kuilazimu Myanmar kuutekeleza.

Katika taarifa jana usiku, wizara ya mambo ya kigeni ya ilisema imeupokea uamuzi huo lakini haikutaja hatua maalum inazochukua. 

Wakati hatua hizo zina kisheria, hakuna mfumo uliowekwa wa kuzitekeleza.

Katika taarifa zilizotolewa tofauti leo, Uingereza na Malaysia zimeitaka Myanmar kuzitekeleza kikamilifu hatua hizo. Msemaji wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Liz Throssell ameuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva kuwa ofisi yake "inatoa miito kwa Myanmar kuzitekeleza kikamilifu haraka na bila masharti.”