1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yatoa msamaha kwa wafungwa

14 Julai 2009

Utawala wa kijeshi wa Myanmar umetangaza kutoa msamaha kwa wafungwa wakiwemo wa kisiasa ikiwa ni siku chache tu baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuutaka umwachie huru kiongozi wa upinzani Aung San Kyi

https://p.dw.com/p/Iokq
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

Balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa Than Swe akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja huo, alisema serikali yake inajiandaa kutoa msamaha kwa wafungwa wa kisiasa katika misingi ya kibinaadamu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujayo.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wiki iliyopita alizuru Myanmar ambapo alitoa wito kwa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo kumuachia huru kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi na kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka ujayo unakuwa halali na huru.


Hata hivyo wakati akitangaza mpango wa kutoa msamaha huo, Balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa hakutaja majina ya wale wanaokusudiwa kufaidika na hatua hiyo.


Lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepongeza hatua hiyo akisema inatia moyo na kuongeza kuwa ataendelea kufuatilia kwa karibu kuona ni kwa jinsi gani utawala huo unatekeleza yale aliyouomba uyashaghulikie.Amesema kuwa hana uhakika kama kiongozi wa upinzani ni miongoni mwa wale watakaofadika na msamaha huo.


Mapema Ban Ki-moon alitoa taarifa kwa wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusiana na ziara yake hiyo huko Myanmar, hivi karibuni, ambapo aliweka wazi kuwa ili uchaguzi nchini Myanmar uonekani huru na kuheshimiwa ni lazima kwa wafungwa wote wa kisiasa akiwemo Aung Sa Suu Kyi waachiwe huru.


Aidha alielezea kusikitishwa kwake na hatua ya utawala wa kijeshi wa nchi hiyo kumzuia kuonana na Bibi Aung Saa Suu Kyi.


´´Hatua ya uongozi wa myanmar kukataa kuniruhusu kukutana na Aung Sa Suu Kyi, siyo tu ni hatua ya kusikitisha lakini pia ilikuwa ni kuinyima Myanmar nafasi muhimu.Kwa kufanyika mkutano huo kati yangu na Suu Kyi, ingekuwa ni kutoa ishara ya mafanikio na maridhiano ndani na nje ya Myanmar´´alisema Ban


Wanachama wa Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa hususani wa nchi za magharibi wameunga mkono matakwa yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa umoja huo kwa utawala wa kijeshi wa Myanmar.


Mjumbe wa Marekani katika baraza hilo Rosemary DiCarlo amesema hakutakuwa na uchaguzi huru na haki iwapo Aung Sa Suu Kyi na wafungwa wengine wa kisiasa zaidi ya elfu mbili hawataachiwa huru.


Naye Naibu Balozi wa Uingereza katika baraza hilo la usalama Philip Parham ameushutumu utawala wa kijeshi wa Myanmar kwa kushindwa kuitumia ziara ya Ban na hivyo kuzidi kujiweka katika nafasi ya kutengwa zaidi.


Balozi wa Ufaransa Jean Maurice Ripert alilitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua kali dhidi ya Myanmar iwapo bibi Aung Sa Suu Kyi hatoachiwa huru.


Mjini Yangon chama cha kiongozi huyo wa upinzani cha National League for Democracy kimesema kina wasi wasi kama kweli utawala huo wa kijeshi utamwachia huru kiongozi wao katika msamaha uliyotangazwa.


Birma / Aung San Suu Kyi auf Poster
Aung San Suu KyiPicha: AP

Kiongozi huyo wa upinzani amekuwa katika kifungo cha nyumbani kwake na kwa sasa gerezani kwa takriban miaka 13 toka utawala huo wa kijeshi ulipokataa kuutambua ushindi wa chama chake hicho cha National League for Democracy mwaka 1990.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Josephat Charo