Myanmar: Viwanja viwili vya ndege vya jeshi vyashambuliwa
29 Aprili 2021Mashambulizi hayo yamefanyika baada ya miezi mitatu ya mzozo nchini Myanmar, uliotokana na mapinduzi ya kijeshi ya Februari mosi. Hadi sasa hakuna kundi lililokiri kuhusika na mashambulizi hayo na hakuna watu walioripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na jeshi la nchi hiyo, roketi nne ziliulenga uwanja wa jeshi ulio katikati mwa mji wa Magway. Hatua za tahadhari zaidi za usalama ziliongezwa katika barabara za nje ya uwanja huo mara baada ya milipuko hiyo.
Baadaye, roketi tano zilirushwa katika uwanja wa Meiktila ambao ni moja ya viwanja vikubwa vya jeshi nchi humo. Tangu serikali ya mshindi wa tuzo ya amani ya Amani Aung San Suu Kyi iliyowekwa madarakani na wananchi ilipopinduliwa, watu wanaounga mkono demokrasia wameitikisa miji kwa kufanya maandamano.
Jeshi la nchi hilo nalo limekuwa likikabiliana na waandamanaji hao kwa kutumia nguvu kubwa ambapo kwa mujibu wa makundi ya wanaharakati, karibu watu 756 wameuawa. Mapambano kati ya jeshi na makundi ya waasi kutoka katika makabila ya walio wachache, yamekuwa yakipamba moto tangu mapinduzi ya kijeshi yalipofanyika huku jeshi likifanya mashambulizi kadhaa ya anga katika maeneo ya mipakani kaskazini na mashariki mwa Myanmar.
Matumaini ya kumaliza mzozo yamefifia
Wakati hali ya machafuko ikiendelea nchini humo na matumaini ya kupata ufumbuzi wa mgogoro huo yakififia, mashambulizi yanayolenga majengo ya jeshi katika eneo hilo ni machache.
Hali mbaya ya usalama nchini Myanmar inaendelea kushika kasi huku matumaini yaliyowekwa kwa nchi jirani wanachama wa mataifa kusini mashariki mwa Asia ASEAN katika kusaidia pata ufumbuzi wa mzozo huo yakipotea.
Nchi kumi wanachama wa umoja huo walifanya mkutano na kiongozi wa juu wa jeshi Jenerali Min Aung Hlang Jumamosi iliyopita katika mji mkuu wa Indonesia na kutangaza kuwa walikubaliana katika maeneo matano ikiwa ni hatua ya kukomesha machafuko na kuhamasisha mazungumzo kati ya jeshi na raia.
Lakini wanajeshi hao walikataa mapendekezo hayo wakisema watayatilia maanani pale tu hali itakapoimarika na walitoa pia mapendekezo yao ya kufanikisha utawala wao.