Mzozo kati ya Saudi Arabia na Lebanon waendelea
10 Novemba 2017Kwa mujibu wa msemaji wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, Waziri Sigmar Gabriel alimweleza kwenye mazungumzo yao kwa njia ya simu mwenzake wa Saudi Arabia Adel al Jubeir kufuatia kujiuzulu kwa Saad al Hariri hali hiyo inatazamwa kwa wasiwasi mkubwa na serikali ya Ujerumani. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia amezungumza na Saudi Arabia pamoja na Iran na kuzitaka nchi hizo zisichangie kuzorota utulivu wa kisiasawa nchini Lebanon.
Rais wa Lebanon Michel Aoun katika ujumbe wake wa kwanza tangu kujiuzulu waziri wake mkuu Saad al Hariri amesema hali kuambatana na jinsi alivyojiuzulu Hariri siku ya Jumamosi iliyopita tena kwa ghafla inabidi itolewe maelezo kutoka upande wa Saudi Arabia. Rais huyo wa Lebanon ameeleza pia wasiwasi wake juu ya kuendelea kubakia nchini Saudi Arabia waziri wake mkuu aliyejiuzulu Saad al Hariri. Shirika la habari la taifa la nchini Lebanon NNA limeripoti kwamba Saad al Hariri anazuiliwa ndani ya nyumba huko nchini Saudi Arabia. Kuna taarifa pia kwamba Hariri ambaye pia ana uraia pacha wa Lebanon na Saudi Arabia anazuiwa bila ridhaa yake nchini Saudi Arabia tuhuma ambazo zinapingwa vikali na nchi hiyo.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Yves Le Drian amesema serikali ya Ufaransa inaamini kuwa waziri mkuu wa Lebanon Saad al Hariri yuko huru na wala hajazuiwa nchini Saudi Arabia. Alisafiri hadi Abu Dhabi siku moja kabla ya ziara ya rais Macron kwa hivyo sisi tunaamini yuko huru na hivyo ana haki ya kujiamulia na kuchagua anachokitaka.
Hapo jana Alhamisi, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema kuwa muwakilishi katika ubalozi wa Marekani mjini Riyadh alikutana na Hariri lakini hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu hali halisi ya Saad al Hariri nchini Saudi Arabia. Mwanasiasa mashuhuri nchini Lebanon Walid Jumblatt amesema Saudi Arabia haipaswi kuilaumu nchi yake kwamba Lebanon imetangaza vita dhidi ya Saudi Arabia, amesema kauli hiyo inasikitisha kutokana na kuwa nchi hizo kuwa ni marafiki wa tangu jadi. Waziri wa Saudi Arabia anayehusika na masuala ya Ghuba Thamer al Sabhan mapema wiki hii aliilaumu serikali ya Lebanon kwa kutangaza vita dhidi ya nchi yake na kusema Lebanon pamoja na kundi la Washia la Hezbollah linaoungwa mkono na Iran ni maadui wa Saudi Arabia. Jumblatt amesema ni wakati sasa Saad al Hariri anafaa kurejea nyumbani.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/RTRE/APE
Mhariri: Josephat Charo