Mzozo wa biashara kati ya mataifa ya Latin Amerika na Umoja wa Ulaya
2 Agosti 2005Mzozo huo juu ya ushuru wa ndizi unatokota kati ya Umoja wa Ulaya na Mataifa ya Amerika kusini yanayolima ndizi kwa wingi ambayo yameuunga mkono uamuzi uliotolewa na shirika la biashara duniani WTO.
Shirika hilo limetoa uamuzi kwamba mapendekezo ya Umoja wa Ulaya ya kutaka kutoza ushuru wa kiasi cha dolla 278.3 kwa kila tani ya ndizi zinazoletwa kutoka nje sio halali.
Wasuluhishi watatu waliochaguliwa na shirika hilo la biashara duniani WTO wamepitisha kwamba ushuru wa dolla 278.3 kwa kila tani ya ndizi uliopendekezwa na jumuiya ya ulaya sio halali na kwamba utawatenga wakulima wa ndizi wa mataifa ya Latin Amerika.
Kutokana na hilo Shirika hilo limeutaka Umoja wa Ulaya kupendekeza kiwango cha chini cha ushuru ifikiapo mwezi januari mwakani.
Mfumo wa sasa wa Umoja wa Ulaya umeundwa kuwasaidia wakulima katika nchi za afrika,nchi zilizopakana na bahari ya karibik na Pacifik zilizokuwa koloni za dolla za Ulaya yaani ACP.
Nchi hizo zilikubali kutia saini mkataba wa makubaliano ya nafuu na Umoja wa Ulaya ili kuziwezesha kushindana na wakulima wakubwa wakubwa wa nchi za Latin Amerika , ambao wengi wanashikiliwa na makampuni makubwa ya mabepari wa Marekani.
Lakini nchi tisa za Latin Amerika ikiwa ni Brazil,Costa Rika,Kolombia,Ecuodor,Guantemala,Honduras, Nicaragua,Panama na Venezuela zimetoa changamoto kwa Umoja wa Ulaya katika shirika la biashara duniani WTO mnamo miezi ya Marchi na April zikisema kiwango cha ushuru kilichotolewa huenda kisababisha athari kubwa katika uchumi wao na mauzo.
Nchi hizo za Latin Amerika zinasema ushuru huo haukuambatana na ahadi zilizotolewa na nchi mbalimbali za Umoja wa Ulaya za kuweka kiwango kitakachohakikisha angalau nchi hizo zinazolima ndizi kwa wingi zinaweza kufikia soko la biashara la ulaya.
Wasuluhishi wa shirika la biashara duniani WTO wamekubaliana chini ya mpango wa jumuiya ya Ulaya kwamba Latin Amerika haitoweza kuliendeleza soko lake la hisa.
Corbana,inayowakilisha wakulima wa ndizi wa taifa la Costa Rika imesema maelfu ya watu wa Latin Amerika wanategemea viwanda vya ndizi.
Rais wa Corbana Romano Orlich amesema ameridhika kwa jinsi wasuluhishi wa shirika la WTO walivyoafikiana nao.
Ameongeza kusema wanatarajia kushirikiana na Umoja wa Ulaya kuhakikisha kunapatikana matokeo ya kuridhisha kwa pande zote.
Hata hivyo Wakulima wa ndizi wa mataifa ya ACP walio na gharama kubwa ya uzalishaji bidhaa hiyo wanataka ushuru wa wa ndizi zinazozalishwa na mataifa ya Latin Amerika uongezwe ili kutoa nafasi nzuri kwao ya kushindana.
Latin Amerika tayari inashikilia robo mbili ya masoko ya ulaya na ndio wasambazaji ndizi pekee katika nchi ya Marekani.
Mataifa ya ACP hivi sasa yana asilimia 20 ya hisa katika soko la ndizi la Jumuiya ya Ulaya huku wakulima hasa wa Uhispania wakiwa na asilimia 20 ilhali Latin Amerika inashikilia soko kwa asilimia 60 ya hisa.
Sasa Jumuiya ya Ulaya imebakia na siku tisa za kuanza tena mazungumzo na wakulima wa mataifa ya Latin Amerika juu ya kiwango kipya cha ushuru.
Iwapo hakuna makubaliano yatakayopatikana juu ya suala hilo basi upande wowote ule unaweza kuitisha vikao zaidi vya usuluhishi.