1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Caucasus watishia uhusiano wa Marekani na Urusi

Hamidou, Oumilkher14 Agosti 2008

Urusi yaitaka Marekani ichague kati ya kuiunga mkono Georgia na kuendeleza ushirikiano katika mada muhimu za kimataifa

https://p.dw.com/p/ExLt
Wanamgambo wanaopigania kujitenga jimbo la Ossetia ya kusiniPicha: AP


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,Condoleezza Rice amewasili Ufaransa kwa mazungumzo pamoja na rais Nicholas Sarkozy kuhusu ugonvi kati ya Urusi na Georgia,katika wakati ambapo Washington inapaza sauti dhidi ya Rashia na Moscow nayo ikiitaka Washington ichague kati ya kuiunga mjini Tblissi na ushirikiano pamoja na Urusi.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amewasili katika mji wa kusini wa Ufaransa Toulon kwa mazungumzo pamoja na rais Sarkozy katika kasri la Fort de Brégansson.Mazungumzo yao yanahusiana na mpango wa amani wa vifungu sita ulioshauriwa na Ufaransa kama mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya .Mpango huo uliokubaliwa na Moscow na Tblissi unaonyesha kulega lega hivi sasa.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa,Bernard Kouchner anatazamiwa pia kushiriki mazungumzoni kabla ya kurejea Paris pamoja na waziri mwenzake wa Marekani.


Baadae waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atakwenda Georgia kwa mazungumzo pamoja na rais Mikhail Saakachvili.Ziara hiyo imelengwa kushadidia "mshimakano" wa Washington kwa jamhuri hiyo ya zamani ya Usovieti katika eneo la Caucasus,inayozidi kudai uungaji mkono wa washirika wake dhidi ya Moscow.


Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani nchini Georgia inabainisha azma ya Marekani ya kudhibiti hatamu za kidiplomasia baada ya kumuachilia uwanja rais Nicholas Sarkozy kwa niaba ya Umoja wa ulaya.


Ufaransa imewatolea mwito wanachama wengine wa baraza la usalama "waunge mkono haraka" mswaada wa azimio unaojumuisha pia makubaliano ya amani kati ya Urusi na Georgia,ili kuyapa nguvu makubaliano ya kuweka chini silaha.


Wakati huo huo sauti zinazidi kupazwa mijini Washington na Moscow.Akitangaza uamuzi wa kumpeleka waziri wake wa mambo ya nchi za nje katika eneo la Caucasus,rais George w. Bush aliitaka Urusi iheshimu ahadi ilizotoa za kusitisha harakati zote za kijeshi nchini Georgia na kuwarejesha nyumbani wanajeshi wake wote walioingia Georgia mnamo siku za hivi karibuni."


Na kabla ya kuondoka kuelekea Ufaransa waziri wake wa mambo ya nchi za nje Condoleezza Rice aliionya Urusi akisema "itajikuta ikizidi kutengwa kimataifa ikiwa haitoheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha."


"Hatuko mwaka 1968 Urusi ilipoivamia Tchekoslovakia ,ikiwatia kishindo majirani zake ,na kuukalia mji mkuu pamoja na kuipindua serikali bila ya shida yoyote" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.


Hivi punde waziri mwenzake wa Urusi Serguei Lavrow amepandisha sauti akisema "Marekani itabidi ichague kati ya kuiunga mkono Georgia na ushirikiano pamoja na Moscow katika masuala ya kimataifa."Waziri Lavrow ameendelea kusema:



"Wote wanazungumzia hayo hayo,kwamba Georgia ya leo ni mradi maalum wa Marekani.Tunaelewa Marekani inataka kuushughulikia mustakbal wa mradi huo.Lakini serikali ya Marekani inabidi ichague kati ya mradi huo wa kuazia na ushirikiano katika masuala muhimu ya kimataifa."


Vyombo vya habari vya Urusi vinahisi mzozo wa Georgia umemaliza enzi za uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya Urusi na Marekani.