Mzozo wa Gaza- Ban Ki-Moon atoa onyo kali.
13 Januari 2009Hii ni baada ya wanajeshi hao kufanya mashambulizi makali ndani ya Gaza ambapo sasa wanakaribia kuuzingira kabisa mji huo.
Mashambulizi makali yalitokea katika barabara za Mji wa Gaza na kusababisha Wapalestina 42 kuuawa ikiwa ni pamoja na wanachama 30 wa kundi la Hamas.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Kii Moon anaelekea eneo hilo la Mashariki ya kati katika juhudi za kukomesha vita hivyo baada ya pande hizo mbili kukataa azimio la Umoja wa mataifa la kusitisha mapigano wiki iliyopita.
Katibu huyo mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Kii Moon alisisitiza kuwa ujumbe anaopeleka katika eneo la mashariki ya kati ni kukomeshwa mara moja kwa vita na kuheshimiwa kwa maazimio ya umoja huo.
Mzozo ambao sasa umeingia siku yake ya 18 na kusababisha vifo vya Waplestina 900 na wengine 4000 kujeruhiwa asilimia 40 ya waliouawa wakiwa watoto na kinamama.
Ziara ya katibu mkuu huyo anayeonekana kukasirishwa na kuendelea kwa mashambulizi hayo baada ya Israel na chama cha Hamas kukataa azimio la umoja wa mataifa la kusitisha mapigano, inakusudiwa kumepeleka hadi Misri, Jordan, Israel, Palestina, Uturuki, Lebanon, Syria na Kuwait kufanya mashauriano na vingozi hao wa mataifa ya kiarabu.
Jamii ya kimataifa hivyo basi inasubiri kwa hamu kuona iwapo ziara ya katibu mkuu huyo itazalisha matunda na hatimaye kukomeshwa vita hivyo na kuwaepushia dhidi raia wa Gaza.
Israel iliendelea na kutekeleza mpango wa kusitisha mashambulizi wa muda wa saa 3 ili kutoa nafasi ya misaada ya kibinadamu kufika Gaza. Kwa mujibu wa mashirika ya misaada ya kibinadamu zaidi ya malori 150 yalitarajiwa kuingia Gaza wakati wa muda huo ili kuwanusuru maelfu ya wakaazi wa Gaza wanaokabiliwa na hali ngumu.
Misaada hiyo ni pamoja na chakula madawa na mafuta ya petroli yanayokusudiwa jenereta za hospitali mjini Gaza zilizokatiwa huduma za umeme. Mashirika hayo yamerejea kutoa huduma katika eneo hilo baada ya kusimamisha shughuli zake kufuatia kushambuliwa kwa wafanyi kazi wake.
Hali hiyo inafuatia mashambulizi makali ya usiku kucha ambapo wanajeshi wa Israel wameuzingira mji wa Gaza na vitongoji vyake.
Jeshi hilo la Israel linasema kuwa limewaua wapiganaji 30 wa Kipalestina waliokuwa wamejificha kwenye mahoteli na misikiti wakati wa oparesheni hiyo iliyosababisha mapigano makali katika barabara za mji wa Gaza wenye idadi kubwa ya watu. Wafuasi wa chama cha Hamas pia walirusha maroketi 30 ndani ya Israel ingawa hakuna habari zozote kuhusu majeruhi.
Israel bado haijaitikia wito na juhudi za kimataifa kutatua mzozo huo ikisisitiza kuwa oparesheni hiyo iliyoingia awamu yake ya tatu huenda ikakamilika hivi karibuni.Msemaji wa serikali ya Israel Mark Regev alisema kuwa, lengo si kukomesha mapigano tu bali kuhakikisha kuwa amani inadumu katika ukanda wa Gaza.
Huku hayo yakijiri Mashauri kuhusu mpango wa amani unaoongozwa na Misri uliendelea mjini Cairo na kuongozwa na Rais Hosni Mubarak. Wajumbe wa chama cha Hamas kwenye mashauriano hayo walitarajiwa kukutana na mpatanishi mkuu kwenye mpango huo Omar Suleiman kujadilia mapendelezo yaliyowasilishwa.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni chama cha Hamas kukomesha mashambulizi ya maroketi kwa Israel, kusitishwa kwa oparesheni ya jeshi la Israel ndani ya Gaza, kusimamiswa kwa njia zinazotumiwa na Hamas kuingiza silaha kimagendo kabla ya kufunguliwa kwa maeneo ya mpakani.
Mapendekezo hayo yanaonekana kukubaliwa na upande wa Israel ingawa Hamas wanasema kuwa baadhi ya vipengee vinahitaji kufanyiwa marekebisho.
Wakati huo huo Rais Mahmud Abbas amema kuwa atahudhuria mkutano wa viongozi wa kiarabu kuhusu mzozo wa Gaza utakaoandaliwa mjini Doha Qatar ijumaa wiki hii. Huu ni mkutano wa tatu kuitishwa nchini Qatar tangu vita hivyo vianze disemba 27.
Mkutano wa awali haukufanyika baada ya Misri kutofautiana vikali kuhusu ajenda ya mkutano huo. Mataifa ya Kiarabu yamegawanyika kuhusu kuunga mkono chama cha Hamas kilichochukua usimamizi wa eneo la Gaza kutoka kwa rais wa Palestina Mamhud Abbas mwaka wa 2007.