Mzozo wa Katalonia na wa Uturuki Magazetini
9 Oktoba 2017Tunaanzia Uhispania ambako mzozo unazidi makali kati ya wale wanaopigania kujitenga na wale wanaopinga kujitenga jimbo tajiri la kaskazini mashariki la Katalonia. Stuttgarter Zeitung linaumulika mzozo huo upande wa kisheria na kuandika: "Hata kama fakhari ya wakataloni inaeleweka lakini kisheria , juhudi zao za kutaka kujitenga na Uhispania si halali. Ingawa watu wanapenda kuzungumzia kuhusu uhuru wa kujiamulia mambo yao, lakini uhuru huo hauzungumzii haki ya kujitenga. Jambo hilo lingewezekana kama Uhispania ingeunga mkono mtengano au kama wakataloni wanakandamizwa kupita kiasi. Hakuna, si la mwanzo na wala si la pili lililotokea. Kwa hivyo hoja za waziri mkuu Rajoy ni sawa. Lakini kwakua msimamo wa serikali ya mjini Madrid ndio ulio sawa, inabidi iridhie pia kujadiliana."
Puigdemond amedhamiria kusababisha vurugu
Maoni sawa na hayo yameandikwa pia na gazeti la mjini Mainz "Allgemeine Zeitung. "Wanaopigania uhuru wanajichimbia kaburi lao wenyewe. Puigdemont haonyeshi kama anavutiwa na ufumbuzi wa kidiplomasia. Kama ndio hivyo asingependekeza umoja wa Ulaya uingilie kati. Kwasababu hakuna wakati wowote ambapo Umoja wa Ulaya utaunga mkono mtengano. Kiongozi huyo wa serikali ya jimbo amefanya hivyo kwasababu anataka kuwavurugia wakaazi wa Umoja wa Ulaya uhuru wao wa kimsingi. La kama sivyo asingeilinganisha hali ya mambo na ile iliyoko nchini Uturuki au Hungary. Upuuzi mtupu au pengine amedhamiria kuzusha vurugu?"
Uturuki yauma na kupuliza
Hali nchini Uturuki inazidi kuzusha wasi wasi. Wanaharakati wa shirika la kimataifa la haki za binaadamu, wakiwemo pia raia wa Ujerumani, wanakabiliwa na kitisho cha kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 15 jela. Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linaandika: "Siasa ya nje tangu ya enzi za Ottman mpaka za Uturuki yenyewe inajulikana tangu takriban miaka 200 sasa. Kijuu juu wanajitokeza kama wasuluhivu na kuonyesha moyo wa kutaka kumaliza mivutano. Wakati huo huo, kutokana na vitendo vyao wanadhihirisha hawako tayari hata kidogo kufikia maridhiano. Hilo limedhihirika katika mahojiano yaliyofanywa na waziri wa mambo ya nchi za nje Mevlüt Cavusoglu mwishoni mwa wiki. "Haoni sababu ya kuwepo mvutano kati ya Ujerumani na Uturuki" alisema katika mahojiano hayo. Wakati huo huo lakini serikali ya Uturuki haizingatii hata kidogo uwezekano wa kuwaachia huru raia wa Ujerumani wanaowashikilia kama mateka wa kisiasa. Kinyume kabisa: Mwendesha mashitaka mkuu ameshauri mwanaharakati wa haki za binaadam Peter Steudtner afungwe miaka 15 jela."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga