Mzozo wa kudumu — Miaka 40 tangu kuanza kwa vita vya Iran-Iraq
Vita vya Iran-Iraq ni mmoja ya mizozo mibaya zaidi ya kijesi ya Mashariki ya Kati. Mzozo huo uliodumu kwa miaka 8, ambamo silaha za kemikali zilitumiwa, uliua maelfu ya watu na kuigawa kanda kwa misingi ya madhehebu.
Mabishano ya ardhi
Septemba 22, 1980, kiongozi wa Iraq Saddam Hussein alituma majeshi katika nchi jirani ya Iran, na kuanzisha vita mbaya iliyodumu kwa miaka minane ambamo maelfu ya watu waliuawa. Vita hiyo ilianzia kwenye mzozo juu ya ardhi kati ya mataifa hayo mawili yenye waumini wengi wa Kishia.
Mapatano ya Algiers
Miaka mitano kabla, mnamo Machi 1975, Hussein, wakati huo makamu wa rais wa Iraq, na Shah wa Iran walisaini makubaliano mjini Algiers kutatua mzozo wa mpakani. Baghdad hata hivyo, iliituhumu Tehran kwa kupanga njama ya mashambulizi na ikatoa wito wa kuondolewa watu kwenye visiwa viwili vya kimkakati katika njia ya bahari ya Hormuz, vilivyodaiwa na mataifa yote mawili pamoja na UAE.
Chanzo muhimu cha maji
Septemba 17, 1980, Baghdad iliyatangaza makubaliano ya Algiers kuwa batili na ikadai udhibiti wa Shatt al-Arab yote - mto wenye urefu wa kilomita 200 unaotengenezwa kwa kukutana Tigris na Euphrates, ambayo inatiririka kwenye ghuba.
Mashambulizi ya bandari na miji
Vikosi vya Hussein vilishambulia viwanja vya ndege vya Iran kwa mabomu, kikiwemo cha Tehran, pamoja na miundombinu ya kijeshi na mitambo ya mafuta. Vikosi vya Iraq vilikumbana na upinzani mdogo katika wiki ya kwanza na viliteka miji ya Qasr-e Shirin na Mehran, pamoja na bandari ya kusini-magharibi mwa Iran ya Khorramshahr, ambako mto Shatt al-Arab unakutana na bahari.
Adui wa pamoja
Mataifa mengi ya Kiarabu, zikiwemo Saudi Arabia na Kuwait, yaliiunga mkono Baghdad katika vita dhidi ya Iran, yakihofia kwamba mapinduzi ya Kiislamu yalioongozwa na Ayatollah Khomeini yangeweza kuwashawishi waumini wa Kishia katika Mashariki ya Kati. Mataifa ya Magharibi pia, yaliisaidia Baghdad na kuuza silaha kwa utawala wa Hussein.
Iran yajibu mashambulizi
Mashambulizi ya kujibu ya Iran yaliishtua Iraq, baada ya Tehran kufanikiwa kurejesha udhibiti wa bandari ya Khorrramshahr. Baghdad ilitangaza kusitisha mapigano na kuondoa vikosi vyake, lakini Tehran ilikataa mpango huo na kuendelea kuishambulia miji ya Iraq. Kuanzia Aprili 1984, pande mbili zilishiriki "vita vya miji", ambamo miji ipatayo 30 kwa kila upande ilishambuliwa kwa makombora ya masafa.
Silaha za kemikali
Moja ya matukio makuu ya vita vya Iran-Iraq lilikuwa matumizi ya Baghdad ya silaha za kemikali dhidi ya Iran. Tehran ilianza kutoa madai hayo 1984 - na kuthibitishwa na UN - na kisha tena mnamo 1988. Juni 1987, vikosi vya Iraq vilidondosha mabomu ya gesi katika mji wa Iran wa Sarasht. Machi 1988, Iran ilidai kwamba Baghdad ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Iraq katika mji wa Halabja.
Mapatano
Julai 18, 1988, Khomeini alikubali azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumaliza vita. Wakati idadi halisi ya waliouawa katika vita hiyo haijulikani, watu wasiopungua 650,000 walikufa wakati wa mzozo huo. Makubaliano ya kusitisha mapigano yalitangazwa Agosti 20, 1988.
Ukurasa mpya
Kuondolewa kwa utawala wa Hussein na Marekani mwaka 2003, kulianzisha zama mpya katika Mashariki ya Kati. Uhusiano kati ya Iraq na Iran umeboreka tangu wakati huo, na mataifa hayo mawili yanazidi kushirikiana katika nyanja za kiuhumi, kitamaduni na kijamii.