Mizozo yagubika mkutano wa viongozi wa Ulaya na Ghuba
17 Oktoba 2024Viongozi wa nchi za Ghuba akiwemo Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman jana walikutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji kwa mazungumzo ambayo walitumai yangesaidia kutuliza mvutano unaozidi kuongezeka Mashariki ya Kati. Umoja wa Ulaya unajaribu kushirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Ushirikiano la nchi za Ghuba GCC, kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati na Ukraine.
Pande zote mbili zilitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano nchini Lebanon na kulaani mashambulizi dhidi ya vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Mkutano huo wa kwanza na wa aina yake baina ya Umoja wa Ulaya na viongozi wa nchi za Ghuba umefanyika kuelekea mkutano wa viongozi wa Ulaya utakaofanyika mjini Brussels. Masuala mengine yaliyojadiliwa ni biashara, nishati na mabadiliko ya tabia nchi.