Mzozo wa Nagorno-Karabakh unazidi kufukuta
15 Oktoba 2020Rais wa Azerbaijan ameonya juu ya waathiriwa wapya na umwagaji damu zaidi kutokana na mapigano katika eneo linalozozaniwa la mlima yalioanza Septemba 27.
Matumaini ya kusitisha mapigano katika mzozo wa Nagorno Karabakh yanazidi kudidimia katika wakati ambapo idadi ya vifo katika mapigano hayo ikiongezeka huku Armenia na Azerbaijan wakinyoosheana kidole cha lawama, kila mmoja akimshutumu mwenzake kwa kuanzisha mashambulizi mapya.
Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev ametaika Armenia kusimamisha juhudi za kuchukua umiliki wa majimbo yaliokombolewa. Aliyev amesema nchi yake itachukua mikoa yote ya Nagorno-Karabakh iwapo Armenia ''itakosea njia.''
Hatua ya kutaka pande hizo zinazohasimiana kuweka chini silaha iliyoafikiwa Jumamosi iliyopita kwa lengo la kuruhusu pande hasimu kubadilishana wafungwa na miili ya watu waliouawa katika mapigano hayo, inaonekana kuwa na athari ndogo juu ya mapigano karibu na Nagorno-Karabakh, jimbo linalotaka kujitenga ambalo liko ndani ya Azerbaijan, lakini linaongozwa na watu wenye asili ya Armenia.
Katika mapigano mabaya zaidi tangu vita vya miaka ya 1990 vilivyosababisha vifo vya kiasi ya watu 30,000, mamlaka za Armenia zinasema wanajeshi 604 wa Nagorno-Karabakh wameuawa.
Kupitia mtandao wake wa Twitter, msaidizi wa Rais wa Azerbaijan, Hikmet Hajiyev ameandika kuwa raia watatu wa Azerbaijan waliuawa na wengine watatu wamejeruhiwa wakati wa mazishi katika eneo la Terter.
Idadi hiyo inaongezea makadirio ya Azerbaijan yaliyotolewa Jumatano kuwa raia 43 wameuawa hadi kufikia sasa. Hata hivyo, nchi hiyo haitoi takwimu zozote za majeruhi wake wa kijeshi. Ofisi ya mwendesha mashtaka imesema mapema Alhamisi kuwa raia wawili wamejeruhiwa katika eneo la Aghdam.
Mashirika ya kimataifa likiwemo kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu yameonya kuwa mzozo huo ambao unatokea kipindi hiki cha janga la virusi vya corona, huenda ukasababisha maelfu ya watu kuhitaji misaada ya dharura katika muda wa miezi ijayo.