Mzozo wa Qatar watanda magazeti ya Ujerumani
8 Juni 2017Gazeti la Süddeutscher Zeitung linaandika kuwa imedhihirika wazi sasa kwamba kwa Kansela Angela Merkel na naibu wake, Sigmar Gabriel, hakuna tena nafasi ya majadiliano na Uturuki.
Ingawa kila upande unataka kuwa mshindi, lakini Wajerumani wanadhani wamewaonesha Waturuki kwamba hawawezi kuchezewa masharubu. Na Waturuki nao wanataka kuthibitisha msimamo wao: kwamba yeyote anayewahifadhi wale inaowaita kuwa magaidi, basi hawezi kuhesabiwa kuwa mshirika wa dhati.
Hata hivyo, linaandika gazeti hilo, "kuvunjika kwa kambi ya kijeshi ya Incirlik hakumaanishi kuvunjika kwa mashirikiano mengine kati ya mataifa hayo mawili." Bado kuna masuala kadhaa ambayo Ujerumani na Uturuki zina makubaliano ya ushirikiano na ni vigumu kumalizika kwa namna hii hii ya Incirlik.
Mashambulizi ya kigaidi Tehran
Suala jengine kubwa kwenye magazeti ya leo (Juni 8) ni mashambulizi ya jana katika mji mkuu wa Iran, Tehran, ambako mshambuliaji wa kujitoa muhanga na wenzake kadhaa wenye bunduki waliuwa watu wanane katika kaburi la mwasisi wa mapinduzi ya nchi hiyo, Rouhullah Khomenei, na kwenye jengo la bunge.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaandika kuwa kikosi maalum cha kijeshi cha Iran kinasema kuwa Marekani na Saudi Arabia zinahusika moja kwa moja na mashambulizi hayo, ambayo tayari kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) limejibebesha dhamana.
Tuhuma hizi za Iran, linasema gazeti hilo, si za kushangaza, maana siku zote Jamhuri hiyo ya Kiislamu imekuwa ikishikilia msimamo wake kuwa Saudi Arabia ndiye mwasisi na mlezi mkuu wa kundi la IS.
Kwa mashambulizi haya na tuhuma hizi, maana yake ni kuwa hatua za Rais Hassan Rouhani kusaka amani na majirani zake na pia ulimwengu wa Magharibi zinaweza kurejeshwa nyuma.
Mzozo wa kidiplomasia Ghuba
Mada ya mwisho muhimu kwa leo haiendi mbali sana na eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, kwani inahusu mzozo wa kidiplomasia kati ya Qatar, kwa upande mmoja, na mataifa kadhaa ya Kiarabu, ikiwemo Saudi Arabia, Bahrain, na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Hiyo ilikuwa moja ya mada zilizozungumzwa jana katika mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na Ujerumani jijini Berlin, ambapo linaandika gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger kwamba Saudia inazidi kutanua misuli yake mbele ya kijitaifa kidogo cha Ghuba, Qatar, na inaonekana haitakuwa radhi hadi ipate ilitakalo.
Hata hivyo, uingiliaji kati wa Marekani kwenye mzozo huo haukuipendeza Ujerumani, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, alisema wazi kwamba Donald Trump hapaswi kutumia kile alichokiita "utrampushaji" wa mgogoro katika Ghuba, maana hatua yake hiyo inaliingiza eneo hilo kwenye mashindano ya silaha.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Kölner Stadt-Anzeiger, Frankfurter Allgemeine, Süddeutscher Zeitung
Mhariri: Saumu Yussuf