1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Sahara Magharibi wafukuta

5 Aprili 2018

Morocco ameonya kuchukua hatua ikiwemo ya kijeshi kama Umoja Mataifa hautachukua hatua dhidi ya ujenzi na mpango wa chama cha Polisario kuanzisha vituo vya kijeshi katika ukanda usio wa kijeshi katika Sahara Magharibi.

https://p.dw.com/p/2vX1d
Westsahara Konflikt Flüchtlinge im Smara Flüchtlingscamp
Wimbi la kumbukumbu ya wakimbizi la mzozo wa muda mrefu wa Sahara MagharibiPicha: Getty Images/AFP/D. Faget

Waziri wa mambo ya nje wa Morocco Nasser Bourita ameonya kwamba nchi yake inazingatia kuchukua hatua zote ikiwemo ya kijeshi kama Umoja Mataifa hautachukua hatua dhidi ya ujenzi na mpango wa chama cha Polisario kuanzisha vituo vya kijeshi katika ukanda usio wa vita unaosimamiwa na Umoja wa mataifa katika eneo la Sahara Magharibi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Waziri Bourita amesema kwamba makubaliano ya kusitisha vita ya mwaka 1991 yanatishiwa na vitendo vya hivi karibuni vya chama cha Polisario ambacho kinatafuta uhuru wa eneo la Sahara Magharibi lenye utajiri mkubwa wa madini. Nikimnukuu hapa anasema" Morocco inasema wazi kabisa hatua zote zinazingatiwa, Morocco haiwezi kuruhusu mabadiliko kwa makubaliano yaliyopo. Kama Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Kimataifa haziwajibiki, Morocco itachukua majukumu yake."

Kukanisha kwa tuhuma za Morocco

Westsahara Konflikt UNO
Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa katika Sahara ya MagharibiPicha: Getty Images/AFP/F. Batiche

Mapema wiki hii mwakilishi wa Chama cha Polisario katika Umoja wa Mataifa, Ahmed Boukhari alizikanusha tuhuma Morocco kwa kuzieleza kuwa zisizo na msingi na za uongo. Baadae Jumatatu aliliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa katika barua yake kwa kusema jeshi la ulinzi wa amani la Umoja wa Mataifa  katika eneo la Sahara Magharibi halijaripoti taarifa yoyote ya kisa cha kukiukwa kwa makubaliano ya kuweka chini silaha, kilichofanywa na kundi hilo lenye kufanya harakati za kutaka kujitenga.

Boukhari ameituhumu Morocco kwa kutaka kubadili hali ya sasa ilivyo kwa kujenga barabara katika eneo la ukanda salama wa eneo la Guergert. Vilevile amesema tuhuma hizi za sasa za Morocco zina lengo la kuliondosha baraza la usalama katika zingatio la masuala yake yanayosababisha mkwamo kwa kipindi hiki katika eneo la Sahara Magharibi. Jana Jumatano Shirika la habari la Algeria APS lilichapisha taarifa ya Kundi la Polisario ikisema Boukhari amefariki dunia Jumanne nchini Uhispania akiwa na umri wa miaka 64 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Morocco ilichukua udhibiti wa jimbo hilo la Sahara Magharibi mwaka 1975 baada ya mtawala wa kikoloni Kihispania kujiondoa , na kusababisha mapigano ya chini kwa chini kwa ajili ya uhuru wa jimbo hilo ambayo yalimalizika mwaka 1991 wakati umoja wa mataifa ulipoweza kupatanisha na kupeleka jeshi la kulinda amani katika jimbo hilo. Hatua hiyo pia ilikwenda sambamba na kufanyika kwa kura ya maoni kwa ajili ya kuamua hatma ya baadae ya eneo hilo. Hata hivyo kura hiyo haijapigwa mpaka wakati huu.

Morocco inalichukulia eneo la Sahara Magharibi lenye utajiri mkubwa wa madini kama "jimbo lake la kusini" na imependekeza kulipa eneo hilo nguvu kubwa ya kujitawala. Lakini Chama cha Polisario kimeendelea kushinikiza kujitegemea kwa kutumia kura ya maoni kwa watu wa eneo hilo ambao wanakadiriwa kuwa kati ya 350,000 na 500,000. Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Morocco Nasser Bourita anasema amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hapo jana na amemkabidhi barua kutoka kwa Mfalme Mohammed wa Sita ambae pia alizungumza na mkuu huyo wa umoja wa mataifa. Anasema mfalme nae amesitizita kutatuliwa haraka mzozo uliopo tofauti na hapo Morocco itachukua hatua.

Mwandishi: Sudi Mnette APE

Mhariri: Iddi Ssessanga