1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Tigray unaweza kuchochea vurugu za kikabila

21 Julai 2021

Wapiganaji zaidi kutoka mikoa mbalimbali ya Ethiopia wameahidi kwenda kupigana Tigray. Baadhi ya wadadisi wanahofia hii inaweza kuitumbukiza Ethiopia katika mzunguko wa vurugu za kikabila.

https://p.dw.com/p/3xmoQ
Äthiopien Tigray-Krise
Picha: Stringer/REUTERS

Wapiganaji zaidi kutoka mikoa mbalimbali ya Ethiopia wameahidi kwenda kupigana Tigray. Baadhi ya wadadisi wanahofia hii inaweza kuitumbukiza Ethiopia katika mzunguko wa vurugu za kikabila. Wengine wanaiona hatua hiyo kama ishara ya umoja wa Waethiopia.

Vikosi maalumu na wapiganaji kutoka mikoa kadhaa ya Ethiopia vinajipanga kupiga tafu operesheni za jeshi la shirikisho mkoani Tigray, katika ishara ya kupanuka kwa mzozo. Vikosi vya kawaida wa mkoa wa Amhara, vimekuwa vikipambana sambamba na majeshi ya shirikisho tangu waziri mkuu Abiy Ahmed alipoanzisha kampeni ya kijeshi mkoani Tigray Novemba mwaka jana. Lakini sasa wapiganaaji wa kawaida na wasio wa kawaida kutoka mikoa sita ambayo hapo nyuma haikujihusisha na mzozo huo wanajiunga, wakiwemo kutoka Oromia, mkoa wenye wakaazi wengi zaidi, na pia Sidama, Somalia na Southern Nations, Nationalities and Peoples SNNP.

Äthiopien Tigray-Krise | Armee
Askari wa serikali ya EthiopiaPicha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Ethiopia ina mfumo wa shirikisho linaloundwa na mikoa kumi na miji mwili ya kiutawala, ambayo msingi wake kwa sehemu kubwa ni wa kikabila. Kila mkoa una vikosi vyake maalumu, pamoja na makundi ya ndani ya wanamgambo yanayoundwa na wakulima yanayofanana na kikosi cha ulinzi wa ndani. Msimamizi wa zoni ya Gojam Magharibi mkoani Amhara, Simenhe Ayalev, alisema wiki iliyopita kwamba wametuma zaidi ya wapiganaji 2000 katika uwanja wa vita, kwa mujibu wa shirika la habari la Bloomberg. Kjetil Tronvoll, Profesa wa masomo ya amani na mizozo katika chuo kikuu cha Bjorknes nchini Norway, anasema hili ni tatizo kubwa.

"Kisha una kundi la wapiganaji wa kimkoa, ambao kimsingi ni wakulima na wakaazi wa mjini waliopewa Kalashanikov na yumkini mafunzo kidogo. Lakini wanaitwa pia kwa sababu wanahitaji idadi kubwa ya watu ardhini kwasababu vita mpaka sasa vimevisambaratisha vikosi vya serikali. Na hilo ndiyo janga kwamba wapiganaji hao wanaweza kuchukuliwa kama wanajeshi wa kutumia tu dhidi ya adui. Na tunaweza kutarajia idadi kubwa ya vifo huko."

Waziri Mkuu Abiy alitoa wito wa msaada wa kijeshi kutoka mikoani baada ya chama tawala cha zamani cha Tigray, cha Tigray People Liberation Front (TPLF), kurejesha udhibiti wa mji mkuu wa jimbo na kuvifurusha vikosi vya shirikisho mwezi Juni. Uhamasishaji huu wa wapiganaji unakuja katikati mwa ripoti kwamba waasi wa Tigray wanaanza kufanya mashambulizi ndani ya maeneo ya Tigray yanayokaliwa na vikosi vya Amhara pamoja na kwenye mkoa wa Afar, unaopakana na Tigray upande wa mashariki. Wapiganaji wa Tigray walivuka na kuingia Afar siku ya Jumamosi na vikosi vya Afar na vikosi vya Afar na wapiganaji washirika vilikuwa vinaendelea kupambana nao siku ya Jumatatu, msemaji wa Afar Ahmed Koloyta aliliambia shirika la habari la Reuters.

Mchambuzi Yohannes Woldemariam mwenye makao yake nchini Marekani, alisema Afar ni ya kimkakati sana kwa sababu barabara na reli vinavyounganisha mji mkuu Addis Ababa na Djibouti vinapitia huko. Hivyo ikiwa TPLF itafanikiwa kuzuwia reli, serikali kuu haitakuwa na njia ya kuifikia bandari. Melisew Dejene, mwanataaluma kutoka chuo kikuu cha Hawassa nchini Ethiopia, alisema hakushangazwa kuona watu wakija pamoja chini ya bendera moja kulitetetea taifa lao

Äthiopien Tigray Ärzte ohne Grenzen MSF
Wakimbizi wa Tigray Picha: Nariman El-Mofty/AP/picture alliance

"TPLF imegeuka kitisho kwa taifa na kufuatia sheria na amri iliyopitishwa na Baraza la wawakilishi kulitangaza kundi hilo la Tigray kuwa la kigaidi katika sheria ya karibuni. Hivyo nadhani haishangazi kuona vikosi tofauti kutoka mikoa tofauti vikija pamoja kutetea maslahi ya kitaifa."

Taifa hilo la pembe ya Afrika lenye idadi ya watu wapatao milioni 110, lina zaidi ya makundi 80 ya kikabila. Kulingana na mataalamu wa mizozo Kjetil Tronovoll hata hivyo, baadhi ya mikoa ilikuwa na mijadala mikali ya ndani kuhusu iwapo wanapaswa kuitikia wito wa Abiy kwenda Tigray. Tronovoll anaamini mzozo huu unatazamwa ndani ya Ethiopia kama vita vita kati ya Amhara na Tigray. Mzozo unaongezwa ugumu zaidi na uingigiliaji wa wanajeshi kutoka taifa jirani la Eritrea, waliokuja kuisadia serikali ya Abiy. Kiongozi wa Eritrea, Isaias Afwerki, ni adui mkubwa wa TPLF, iliyoitawal Ethiopia wakati mataifa hayo mawili yalipopigana vita vya mpakani.

Tangu kuondoka kwa wanajeshi wa Ethiopia kutoka Tigray, mkoa huo umekatiwa tena mawasiliano ya simu na intnaeti -- sawa na ilivyokuwa mwanzoni mwa mzozo huo. Na hofu imechochewa zaidi na hotuba ya waziri Abiy alioitoa siku ya Jumapili, ambamo alitumia maneno kama vile, magugu, saratani na ugonjwa, kuilezea TPLF katika ujumbe wa Twitter. Mtaalamu wa mizozo Tronvolla anaiona lugha hii kuwa hatari, inayoelekea kwenye matamdhi ya mauaji ya kimbari.