1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa uongozi wapamba moto PEGIDA

29 Januari 2015

Wajumbe watano wa vuguvugu la PEGIDA lilalopinga Uislamu wamejiuzulu kufuatia utata uliozushwa kutokana na picha za muasisi wa kundi hilo Lutz Bachmann kujifananisha na Hitler na matamshi yake ya kibaguzi.

https://p.dw.com/p/1ESXs
Kathrin Oertel msemaji wa Pegida aliyejiuzulu Jumatano.(28.01.2015).
Kathrin Oertel msemaji wa Pegida aliyejiuzulu Jumatano.(28.01.2015).Picha: picture-alliance/dpa/A. Burgi

PEGIDA kundi la vuguvugu linalojiita Wazalaleno wa Ulayawanaopinga kusilimishwa kwa inakabiliwa na mtihani mkubwa wakati wafuasi wake wakikabili siku ya leo na mshtuko wa kupoteza nusu ya uongozi wake wa juu ambao umejiuzulu.

Wiki moja baada ya kujiuzulu kwa muasisi wa kundi hilo Lutz Bachmann msemaji wa kundi hilo Kathrin Oertel naye amen'gatuka hapo jana na muda mfupi baadae viongozi wenzake wengine wanne wakafuata nyayo zake.

Oertel amejiuzulu kutokana na kile kundi hilo la PEGIDA ilichosema kwamba kutokana na uhasimu mkubwa,vitisho na hasara kwa maisha yake ya kikazi.

Kusambaratika kwa uongozi

Katika taarifa Pegida imesema hata mwanamke awe mkakamavu kwa kiasi gani inabidi atake wakati wa kupumuwa ikiwa usiku wapiga picha na watu wengine wasiojulikana wananyemelea nje ya nyumba yake.

Wafuasi wa Pegida katika mojawapo ya maandamano yao mjini Dresden.
Wafuasi wa Pegida katika mojawapo ya maandamano yao mjini Dresden.Picha: Reuters/F. Bensch

Kiongozi mwengine Volker Lincke ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba ameamuwa kujiuzulu kwa sababu asingeliweza kukubaliana na matamshi ya kibaguzi yanayodaiwa kutolewa na Bachmann.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema Thomas Tallacker mwanachama wa zamani wa chama cha Kansela Angela Merkel CDU ameachia wadhifa wake katika kundi hilo pamoja na naibu wa kundi hilo Rene Jahn.

Achim Exner mwanachama wa chama cha sera kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani AfD inaripotiwa kuwa pia anajiuzulu.Chama cha AfD ambacho kuanzia mwezi wa Augusti kimekuwa kikifaulu kujisombea viti katika mabunge ya majimbo mashariki mwa Ujerumani kwa kiasi fulani kutokana na ilani yake ya kupiga vita wageni kimekuwa miongoni wa waungaji mkono wakubwa kabisa wa Pegida.

Hatari za ubaguzi

Viongozi wa kisiasa akiwemo Merkel wamelaani maandamano ya Pegida wanayofanya nchini na kuonya juu ya hatari za ubaguzi na ukosefu wa uvumilivu katika jamii.

Uongozi wa kisiasa wa Ujerumani umekuwa katika kipindi kigumu kukabiliana na mafanikio ya kundi hilo ambalo limekuwa likiwavutia maelfu ya watu katika maandamano yake ya kila wiki nchini kote.

Mwishoni mwa juma wafuasi wa Pegida walikutana na Sigmar Gabriel kiongozi wa chama cha SPD mshirika mdogo wa serikali ya mseto ya Kansela Merkel. Gabriel pia ni naibu kansela na waziri wa uchumi katika serikali hiyo.

Sigmar Gabriel Naibu Kansela na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani.
Sigmar Gabriel Naibu Kansela na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maziere na Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen ambao wote wawili ni wanachama wa chama cha Merkel cha CDU pia wanaamini kwamba viongozi wa kisiasa wa Ujerumani wanapaswa kuwa na mazungumzo na kundi hilo la Pegida.

Lakini Horst Seehofer ambaye anakiongoza chama ndugu na CDU cha CSU chenye makao yake katika jimbo la Bavaria amekataa kufanyika kwa mazungumzo ya aina yoyote yale na Pegida.

Pia kumekuwepo dalili kwamba kuungwa mkono kwa maandamano ya Pegida yumkini kukawa kumeanza kufifia kutokana na kusambaratika kwa uongozi wake huo wa juu.Pegida imetangaza kwamba imefuta maandamano yake ya kila wiki yaliopangwa kufanyika mjini Dresden Jumatatu.

Mwandishi :Mohamed Dahman/dpa/AFP

Mhariri :Yusuf Saumu