Mzozo wa Urusi na Ukraine Magazetini
27 Novemba 2018Tunaanza na mzozo unaotisha kati ya Urusi na Ukraine baada ya Urusi kuzikamata manuari za Ukraine katika bahari nyeusi nayo Ukraine kutangaza sheria ya hali ya hatari. Gazeti la "Osnabrücker Zeitung" linajiuliza nani wa kulaumiwa kati ya mafahali hao wawili? Gazeti linaendelea kuandika: "Eti nani aitwe mhanga na nani mchokozi? Kila wakati malumbano yanapojiri kati ya Urusi na Ukraine, kila mmoja anaeneza hoja zake. Na nchi za magharibi hazikawii kuitupia lawama serikali ya mjini Moscow. Ukweli lakini pia ni kwamba nchini Ukraine uchaguzi umepangwa kufanyika marchi mwaka 2019. Utafiti wa maoni ya wananchi unaashiria rais Petro Poroschenko hana nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi huo kutokana na uzembe wa serikali yake katika kupambana na rushwa. Sheria ya hali ya hatari inafungua njia ya kupata uungaji mkono wa wananchi katika kukabiliana na adui kutoka nje. Zaidi ya hao mwishoni mwa mwezi wa january vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi vitarefushwa. Kwa hivyo kilichotokea katika bahari nyeusi kinaweza kuchukuliwa kama hoja ya kuilaumu Moscow kuwa ndio mchokozi."
Friedrich Merz ajiponza
Mgombea mmojawapo wa wadhifa wa mwenyekiti wa chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union-CDU, Friedrich Merz anakosolewa baada ya kuhoji kwamba chama hicho cha kihafidhina ndicho kilichowapatia upenu wafuasi wa Chaguo Mbadala kwa ajili ya Ujerumani-AfD wa kupata umashuhuri. Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika: "Hoja za Friedrich Merz, kwamba CDU wamewaachia AfD washinde katika chaguzi tangu katika daraja ya taifa mpaka ya majimbo zinaweza kumgeukia katika kinyang'anyiro cha kuania wadhifa wa mwenyekiti wa chama hicho. Kwasababu kwa kutoa hoja hizo Merz anajitenga na wote wale waliokuwa na majukumu ndani ya chama cha CDU, naiwe kansela, mawaziri wakuu na viongozi wa CDU majimboni. Na bila ya shaka anajitenganisha pia na wafuasi wa CDU mashinani."
Maajabu ya teknolojia ya kuzaliwa mtoto bila ya mbegu za uzazi
Mada yetu ya mwisho inahusu uvumbuzi wa China ambayo teknolojia yake ya tiba imesaidia kuzaliwa mtoto bila ya mbegu asilia za uzazi. Gazeti la Schwäbische Zeitung linaandika: "Kimsingi tukio hilo si chochote isipokuwa kuziendeya kinyume haki za binaadam..Kwamba hujuma hizo zinajiri wiki mbili kabla ya kuadhimishwa miaka 70 tangu haki za binaadamu zilipotangazwa, tukio hilo linadhihirisha jinsi haki hizo zilivyo tete na jinsi ambavyo China haizithamini.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman