1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Naibu Kansela wa Ujerumani afanya ziara ya ghafla Ukraine

18 Aprili 2024

Naibu Kansela na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Robert Habeck, amefanya ziara ya kushtukiza mjini Kyiv kuiunga mkono Ukraine na kujadili hatua ya kulijenga upya taifa hilo kufuatia mashambulizi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4ev0U
Robert Habeck
Naibu Kansela na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Robert Habeck, akiwa ziarani nchini Ukraine.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Ziara hiyo ya Alhamisi (Aprili 18) ilifanyika siku chache baada ya Ujerumani kutangaza kuwa inatuma mfumo wa ziada wa ulinzi wa anga nchini Ukraine baada ya Kyiv kuiomba Berlin kuisaidia katika kukabiliana na mashambulizi ya Urusi.

Ukraine inasema kwamba inaelekea kuishiwa na silaha za kudungua makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi huku Moscow ikizidisha mashambulizi kwenye miundombinu ya nishati.

Soma zaidi: Zelenskiy aishukuru Poland kwa ushirikiano

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell, alisema kwamba nchi za Magharibi zinapaswa kuchukua maamuzi ya haraka ili kuisaidia Ukraine.

"Nchi za Magharibi, Japani, Kanada, Marekani na Ulaya zinapaswa kuchukua maamuzi ya haraka ili kuiunga mkono Ukraine zaidi, kwa sababu hatuwezi kuvumilia ushindi wa Putin nchini Ukraine," alisema Borell.

Soma zaidi: Zelensky ataka NATO kujadili ulinzi wa anga wa Ukraine

Mkuu huyo wa masuala ya kimataifa wa Umoja wa Ulaya alielezea wasiwasi wake kwamba katika siku zijazo maamuzi muhimu "yanapaswa kuchukuliwa ili kutuma mifumo zaidi ya ulinzi wa anga kwa Ukraine, vyenginevyo mfumo wa nishati wa Ukraine utaharibiwa."

Siku ya Jumatano (Aprili 17), Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani alitoa wito kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kufuata mfano wa Berlin na kutuma mifumo zaidi ya ulinzi wa anga nchini Ukraine.