1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Naibu Kiongozi wa LRA kufika mbele ya ICC

Caro Robi21 Desemba 2015

Aliyekuwa naibu wa kiongozi wa waasi wa Lords Resistance Army LRA nchini Uganda, Dominic Ongwen, anafikishwa kizimbani katika mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC. Ongwen alikuwa msaidizi wa kamanda wa LRA Joseph Kony

https://p.dw.com/p/1HQwt
Picha: picture-alliance/epa/P. Dejong

Dominic Ongwen atafikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa inayoshughulikia uhalifu yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, akituhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Upande wa mashitaka unatumai kupata taarifa zaidi kuhusu mfumo wa uongozi wa kundi hilo wakati wa kesi hiyo ya Ongwen.

Ongwen alitekwa nyara na LRA akiwa na umri wa miaka kumi alipokuwa akielekea shuleni na kulazimishwa kuwa mpiganaji wa kundi hilo. Alijipatia umaarufu na kuheshimika katika kundi hilo LRA kwa kufanya mauaji ya kinyama, kupora mali na kubaka kama mfuasi sugu wa Kony na kupandishwa cheo hadi kuwa naibu wa Kony.

Mnamo mwezi Januari mwaka huu, alijisalimisha kwa kikosi maalumu cha jeshi la Marekani waliokuwa wanashiriki katika operesheni ya kumtafuta Kony katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kukabidhiwa kwa ICC.

Ongwen ni muathiriwa au mtuhumiwa?

Kesi dhidi yake itafuatiliwa kwa makini kwa sababu huenda ikaangazia suali la je ni muathiriwa wa uasi wa LRA au ni mtuhumiwa? ICC iliamua kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao wametekwa nyara au kuhusika katika uhalifu wa kivita wachukulike kama waathiriwa.

Kiongozi wa LRA Joseph Kony
Kiongozi wa LRA Joseph KonyPicha: picture-alliance/dpa/Price

Licha ya kuwa Ongwen alikuwa na miaka kumi alipotekwa nyara na LRA, kipindi cha kujisalimisha kwake alikuwa na miaka 32. Ni uamuzi wa mahakama sasa kuamua iwapo anapaswa kutuhumiwa kwa uhalifu alioutenda na ni kwa kiasi gani.

Mwaka 2005, mahakama ya ICC ilitoa kibali cha kukamatwa kwa Kony mwenye umri wa miaka 55 aliyeanzisha LRA mwaka 1986 baada ya kudai kupokea maagizo kutoka kwa Roho Mtakatifu ya kuunda Dola la Kikiristo Uganda kuambatana na Bibilia na amri kumi za Mungu.

Kiongozi wa LRA Joseph Kony au kama anavyojulikana kwa jina la 'Mchinjaji wa Uganda' anasemekana kuwateka nyara zaidi ya watoto 7,000. Kundi lake la LRA linawatumia watoto hao kama wapiganaji na watoto wa kike kama watumwa wa ngono.

LRA imefanya vitendo vya kikatili

Ili kuwazuia wavulana kutoroka kutoka kundi hilo na kurejea vijini mwao, wengi wa watoto hao wanalazimishwa kuwaua mama zao. Wanawake na wasichana wanabakwa na kulazimishwa kuwaoa wapiganaji.

Mmoja wa waathiriwa wa ukatili wa LRA
Mmoja wa waathiriwa wa ukatili wa LRAPicha: picture-alliance/dpa

Waasi hao wa LRA wamevishambulia vijiji, kuwatesa raia kaskazini mwa Uganda na kuwaua takriban watu laki moja tangu walipoanzisha uasi, huku zaidi ya watu milioni mbili wakilazimika kuyatoroka makaazi yao kutokana na mzozo huo.

Lakini mpaka sasa kiongozi huyo waasi ameweza kukwepa mkono wa sheria akiaminika kuwa katika eneo la mpakani aidha, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan au Sudan Kusini.

Mwandishi: Caro Robi/http://www.dw.com/en/manhunt-for-joseph-kony-continues-as-deputy-faces-icc/a-18929930

Mhariri: Daniel Gakuba