Magufuli aagwa na Wazanzibar
23 Machi 2021Katika mfululizo wa kuomboleza na kumuaga aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli, leo ilikuwa ni zamu ya Zanzibar ambako jeneza lenye mwili wa Magufuli lilipokelewa Mjini Unguja majira ya saa 5 asubuhi na viongozi mbalimbali walioongozwa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Hatua hiyo kabla kabla ya kupelekwa uwanja wa Amaan kwa ajili ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho. Ukimya wa ghafla, simanzi, majonzi na vilio vilitawala wakati wa kuupokea mwili katika uwanja wa Amaan, ambapo wananchi wa mikoa yote mitano ya Zanzibar walipata fursa ya kuuaga, huku wengine wakipata kuuona ukipitishwa wakati ukitokea uwanja wa ndege wakati wa kuelekea uwanjani hapo.
Rais Mwinyi amesema Magufuli sio mtu wa kusahaulika
Viongozi wa serikali ya Tanzania na Zanzibar, mabalozi wadogo wanaoziwakilisha nchi zao, mashirika ya kimataifa, wanafamilia na wananchi, walikuja kuungana na kutowa heshima za mwisho ambapo Rais Mwinyi alihutubia na kumuelezea HayatiMagufuli sio mtu wa kusahaulika kwa aliyoyatenda katika uhai wake.
Licha ya jua kali na kukaa muda mrefu nje wananchi hawakuvunjika moyo na walipata nafasi ya kwenda kutoa heshma zao za mwisho bada ya kumalizika sala za kumuombea zilizoongozwa na viongozi wa dini mbalimbali ikiwemo ya Kikrito, Kiislamu na Kihindu. Pamoja na kwamba shughuli hiyo ilifanyika mjini Unguja lakini pia zaidi a wananchi 200 waliwasili katika kisiwa hicho kwa meli wakitokea kisiwani Pemba.
Uamuzi wa kuletwa mwili Zanzibar umetokana na ombi la wananchi la kutaka kupewa fursa hiyo kama walivyopewa wenzao katika mikoa mengine ya Tanzania bara ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, na baadae Mwanza na Geita mkoa ambao Hayati Magufuli atakapomalizia safari yake hiyo ya mwisho katika wilaya ya Chato.
Chanzo: DW