Namna virusi vya corona vilivyoyaathiri maisha Ujerumani
Wakati maelfu ya watu wakithibitishwa kuuguwa virusi vya COVID-19 nchini Ujerumani, mfumo wa maisha umebadilika: kutoka kandanda, safari za ndege, utengenezaji wa magari na hata utamaduni. DW inaliangalia hilo
Fremu tupu madukani
Hofu ya kukosa chakula katika kipindi hiki imesababisha maduka kubakia matupu. Vyakula vya mikebe na karatasi za chooni ndizo zinazonunuliwa kwa wingi. Maswali yanaulizwa iwapo maduka hayo yana bidhaa nyengine za kutosha kuweza kuwafikia watu wasiojiweza.
Bundesliga yaahirishwa
Baada ya kucheza mechi moja bila ya mashabiki, ligi kuu ya kandanda Ujerumani (Bundesliga) imeahirisha michezo yake hadi Aprili 2. Uamuzi huo umechukuliwa wakati kocha wa Paderborn, Steffen Baumgart, na mlinzi Luca Kilian kuthibitishwa kuugua virusi vya COVID-19.
Matamasha ya kitamaduni yafutwa
Shughuli za kitamaduni zimebadilika, huku maonesho makubwa ya kibiashara ya kitalii yakifutwa au kuahirishwa. Maonesho ya vitabu yayni Book Fair yanayofanyika Leipzig na maonesho ya muziki Frankfurt yamefutwa. Madisko, maduka makubwa na majumba ya makumbusho yamefungwa.
Sio homa ya Wuhan
Eneo la chimbuko la virusi hivyo limesababisha kuendelea kuwepo maneno ya kibaguzi katika maeneo yaliyoathirika zaidi na virusi hivyo. Migahawa ya watu kutoka Asia na sio ya Wachina pekee wameripoti watu kujitenga na migahawa hiyo katika nchi zilizoathirika na corona, huku watu walio na asili ya Asia wakibaguliwa.
Usitishwaji wa safari za ndege
Shirika la ndege la Lufthansa la Ujerumani limepunguza maradufu safari zake kufuatia safari za kibinafsi na zile za kibiashara kupungua. Shirika hilo sasa linaomba msaada wa serikali ili kuendelea na majukumu yake hii, ikiwa ni kwa mujibu wa gazeti la biashara la Ujerumani, Handelsblatt.
Athari katika utengenezaji wa magari
Viwanda vya kutengeneza magari nchini China vimefungwa kuanzia mwezi Januari na watengenezaji wakubwa wa magari nchini Ujerumani, kama Volkswagen na Daimler, wamesema uuzaji na utengenezaji wa magari hayo umeathirika kwa virusi vya corona. Na kampuni nyingi zinazotaka bidhaa au sehemu muhimu za magari kutoka China zinazofanya kazi nchini Ujerumani zimekwama.
Kupungua kwa watalii
"Athari katika sekta ya utalii nchini Ujerumani ni kubwa," ameonya Guido Zöllick, mkuu wa taasisi ya mahoteli na migahawa Ujerumani. Tayari kuanzia wiki ya pili ya mwezi Machi, asilimia 76.1 ya wanachama wa taasisi hiyo wameropiti kupungua kwa watalii na kupungua kwa mapato. Bunge la Ujerumani limewapiga marufuku watalii kuzuru jengo la la glasi la Reichtag.
Ukaguzi wa mipakani
Katika juhudi za kusitisha kuenea kwa virusi vya corona, Ujerumani imefunga mpaka wake na Ufaransa, Luxembourg, Switzerland, Austria na Denmark. Poland na Jamhuri ya Czech zilikuwa zimeshaanza ukaguzi wa barabarani kuchukuwa vipimo vya wasafiri wanaotumia barabara kuu ya kutoka Ujerumani.
Shule zote zafungwa
Shule za chekechea na shule za msingi zote nchini Ujerumani zimefungwa. Kufungwa kwa shule hizo kumewaathiri zaidi ya watoto milioni 2.2 walio na umri wa hadi miaka 16, kulingana na Ofisi ya Takwimu ya Ujerumani.