Nani anaweza kumrithi Angela Merkel kama kansela wa Ujerumani?
Muungano wa vyama vya kihafidhina ya CDU-CSU wa Angela Merkel unakaribia kuamua juu ya mgombea wake mkuu wa uchaguzi mkuu wa 2021. SPD tayari na Chama cha Kijani kinasema kitatangaza mgombea wake mnamo Aprili 19.
Armin Laschet
Mwenyekiti wa CDU Armin Laschet, muungaji mkono mkubwa wa Angela Merkel, anaongoza jimbo lenye idadi kubwa ya watu nchini Ujerumani. Wahafidhina mara kwa mara walimdharau mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 60, maarufu kwa imani yake ya ujumuishaji na maelewano. Lakini hivi karibuni, msimamo wake kuhusu hatua za kupambana na janga la Corona umeibua mtafaruku.
Markus Söder
Waziri mkuu huyu wa jimbo la Bavaria mwenye umri wa miaka 54 kutoka chama cha kihafidhina zaidi ya chama cha CSU, amefaidika katika kura za maoni kutokana na msimamo wake mkali katika vita dhidi ya corona. "Bavaria ina nguvu. Bavaria itakua. Bavaria iko imara. Bavaria iko salama ... na itabakia kuwa hivyo ," alisema mwandishi wa habari huyo wa zamani wakati wa alipoanza kazi yake mwaka 2018.
Annalena Baerbock
Akiwa na miaka 40, Annalena Baerbock amekuwa mwenyekiti mwenza wa Chama cha Kijani tangu 2018. Mwanasheria huyo mwenye shahada katika sheria za kimataifa kutoka chuo cha London School of Economics, anaonekana na wafuasi wake kama mikono salama na ufahamu mzuri wa undani kuliko Habeck. Wapinzani wake wanakosoa uzoefu katika utawala au uwaziri na pia anaposhindwa kufanya vyema katika mahojiano.
Robert Habeck
Robert Habeck, 51, ni msemaji mwenye shauku, mwenye uwezo wa kuitumia sauti yake kwenye mazingira yoyote kwa njia ambayo wanasiasa wengi wa Ujerumani hawawezi. Lakini kama watu wengi walio na kipaji hicho walivyo, hotuba zake huwa zinatoka nje ya mada. Ana shahada ya uzamivu katika falsafa na alikuwa mwandishi wa riwaya na vitabu vya watoto kabla ya kuingia kwenye siasa karibu miaka 20 iliyopita.
Olaf Scholz
Kwa kujikuta kinaporomoka kwenye kila uchaguzi, chama cha SPD kiliamua kumueka mtu mkweli badala ya mkali kama mgombea wao mkuu mnamo 2021. Waziri wa Fedha Olaf Scholz, meya wa zamani wa Hamburg, na naibu wa Merkel katika serikali ya mseto, anaonekana kuwa na ufahamu wa kitaalamu. Lakini wengi katika chama chake wanamuona hana uwezekano wa kuwapa nguvu na kuwavutia wanaharakati wa chama hicho.