Nani atamfunga paka kengele katika Bundesliga
18 Septemba 2020Hata mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge amekiri kuwa ubabe wao wa kunyakua mataji manane mfululizo katika Bundesliga sio mzuri kwa shauku ya mvuto katika ligi lakini mwishoni mwa siku ni jukumu la wapinzani hatimaye kufanya kitu na kuwavua taji hilo.
Borussia Dortmund , klabu ya mwisho kabla ya hatua hii ya Bayern kunyakua mfululizo mataji hayo mwaka 2012, ilikuwa na nafasi ya pekee miaka miwili iliyopita wakati walikuwa wakiongoza kwa pointi 9 mwezi Desemba, lakini waliporomoka na kumaliza wakiwa pointi mbili nyuma ya mabingwa hao.
Mwaka jana RB Leipzig iliongoza hadi nusu ya kwanza ya msimu lakini Bayern ilirejea kutoka kuwa nyuma kwa pointi saba muda mfupi kabla ya kuingia mapumzikoni ya majira ya baridi na kutoroka tena na taji hilo kwa kuongoza kwa pointi 13 mbele ya timu iliyoshika nafasi ya pili Borussia Dortmund.
Dortmund, Leipzig, Bayer Leverkusen na Borussia Moenchengladbach ni washukiwa wa kawaida linapokuja suala la klabu ambayo inaweza kuwapa changamoto Bayern Munich, na pia wametajwa kuwa mahasimu wakuu na Rummenigge.
Lakini inaonekana kuwa juhudi za ziada za kibinadamu zinahitajika kuwaangusha mabingwa hao walionyakua mataji matatu msimu huu.
Mshindi asiyeshindika Bayern
Bayern hawajafungwa katika michezo 20 ya ligi, ambamo wameshinda michezo 19, tangu pale waliposhindwa kupata ushindi dhidi ya Leverkusen na Gladbach mwishoni mwa mwezi Novemba na mapema Disemba. Mchezo pekee waliopoteza pointi ni katika sare ya bila kufungana dhidi ya RB Leipzig mwezi Februari.
Kocha wa Gladbach Marco Rose wamefurahishwa kusikia kuwa ni timu inayoweza kuivua ubingwa Bayern lakini wataweza kuweka changamoto ya kweli iwapo watabakia bila ya majeruhi katika kikosi chake.
Iwapo kila mtu atakuwa katika afya njema,sisi ni wazuri sana. "Iwapo kila mtu atakuwa na hali nzuri ya kiafya, naweza kuona kikosi chetu katika nafasi ya kushinda dhidi ya timu yoyote katika ligi," Rose aliwaambia waandishi habari siku ya Alhamis. Kwa mtazamo huu ni habari mbaya kwamba Breel Embolo , Valentino Lazaro , Laszlo Benes na Denis Zakaria ni majeruhi, kama Rose alivyosema: Iwapo wachezaji hao wanne watakuwa nje kwa muda mrefu , ubingwa huenda hautakuwapo.
Kwanza kabisa kutokuwapo wachezaji hao kunaweza kuathiri mchezo wao muhimu wa ufunguzi wa ligi siku ya Jumamosi dhidi ya Dortmund ambao kwa upande wao wanachukua tahadhari kiasi kuliko miezi 12 iliyopita na hawajasema rasmi wanawania ubingwa.
Kama ilivyo Gladbach , Dortmund imeweza kubakisha kikosi chao, ambapo ni Achraf Hakimi tu ndie aliyeondoka kutoka katika kikosi hicho baada ya kumalizika muda wa kuazimwa kutoka Real Madrid.
Ushambuliaji BvB bado uko shule
Dortmund kwa kiasi kikubwa itawategemea vijana ikiwa ni pamoja na Jadon Sancho, Erling Haaland, Giovanni Reyna, Jesus Reinier , Jude Bellingham na Youssoufa Moukoko ambaye ataweza tu kucheza katika kikosi cha kwanza atakapofikisha umri wa miaka 16 katika majira ya mapukutiko mwaka huu mnamo mwezi Novemba.
Lakini kocha ambaye ni mwenye kuchukua tahadhari sana Lucien Favre ameonya kwamba "katika ushambuliaji bado tuko shule" wakati aliomba uvumilivu lakini Dortmund inaonekana kuwa timu bora ambayo inaweza kuivua ubingwa Bayern.
Leverkusen na RB Leipzig ambazo hazijawahi kushinda taji la Bundesliga, zinakabiliwa na hali ya sintofahamu baada ya kupoteza wachezaji bora.
Leipzig ambayo imefikia nusu fainali ya Champions League imeshuhudia mfungaji wake bora Timo Werner akitimkia Chelsea na inaonekana iwapo Hwang Hee Chan na huenda pia Mnorway Alexander Sorloth wanaweza kujaza hilo pengo.
Nahodha Marcel Sabitzer alisema "Haitakuwa rahisi hivyo kushinda ubingwa" na kocha mwenye dhamira Julian Nagelsmann pia ameeleza kwa tahadhari kuhusu hilo.
"Unaweza kuwa na matundu katika utekelezaji wakati unashughulika na kikosi cha vijana. Baadhi ya pointi zitapotea na itakuwa vigumu kufika juu," Nagelsmann alisema.