Nani atamrithi Angela Merkel kama Kansela wa Ujerumani?
SPD tayari imeamua juu ya mgombea wake mkuu kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2021. Lakini katika kambi ya kihafidhina ya Merkel ya vyama vya CDU/CSU nafasi hiyo inaendelea na chama cha kijani bado hakijafanya maamuzi.
Olaf Scholz
Kikiporomoka kila uchaguzi, SPD kiliamua kumteua mtu mwenye uhalisia badala ya mwenye msimamo mkali kama mgombea wao mkuu katika uchaguzi wa 2021. Waziri wa fedha Olaf Scholz, meya wa zamani wa Hamburg anaonekana kuwa mtu asiye na haiba ya ucheshi na mwenye kariba ya uongozi. Wengi katika chama chake wanasema Scholz mwenye umri wa miaka 62 haonekani kuwapa morali waharakati chamani.
Markus Söder
Waziri mkuu wa Bavaria mwenye umri wa miaka 53 kutoka chama ndugu na CDU cha CSU, amefaidika na maoni ya wapigakura kutokana na msimamo wake mkali katika kupambana na virusi vya corona. "Bavaria ni imara. Bavaria itakua. Bavaria ina nguvu. Bavaria ni salama. Hapa ulimwengu bado upo sawa na itakaa hivyo", alisema mwandishi huyo wa habari wa zamani mwanzoni mwa uongozi wake mwaka 2018.
Armin Laschet
Armin Laschet muungaji mkono thabiti wa Angela Merkel, anaongoza jimbo lenye wakaazi wengi zaidi Ujerumani. Wahafidhina wenye nguvu mara kwa mara walimdharau mwanasiasa huyo mcheshi mwenye umri wa miaka 58, maarufu kwa imani yake katika utangamano na maelewano. Lakini hivi karibuni silika yake ya kutoingilia imempelekea kurejesha maneno yake zaidi ya mara moja wakati wa janga la virusi vya corona.
Jens Spahn
Waziri wa afya Jens Spahn, mwanasiasa chipukizi wa chama cha Christian Democrats, amepata umaarufu wakati wa janga la virusi vya corona. Shoga asiejificha mwenye ndoa, akiwa na umri wa miaka miaka 40 na anaemudu vyema lugha ya Kiingereza, Spahn ni mwanasiasa wa kisasa wa kikatoliki wa CDU kuliko vile mtu angeweza kufikiria miaka michache iliyopita.
Robert Habeck
Robert Habeck mwenye umri wa miaka 50, mzungumzaji mahiri, ana sauti na nguvu inayoendana na vuguvugu la mazingira, ambavyo wanasiasa wengi wa Ujerumani hawana. Lakini kama ilivyo kwa watu wengi wenye kipawa kama hicho, hotuba zake huwa zinatoka nje ya mada. Habeck ana shahada ya falsafa na alikuwa mwandishi wa riwaya na vitabu vya watoto kabla ya kuingia kwenye siasa karibu miaka 20 iliyopita.
Annalena Baerbock
Akiwa bado hajafikia miaka 40 hivi, Annalena Baerbock amekuwa mwenyekiti mwenza wa Chama cha Kijani tangu mwaka 2018. Ana shahada katika sheria za kimataifa kutoka chuo cha uchumi cha London. Wafuasi wake wanamuona chaguo salama na mwenye ufahamu mzuri wa maelezo kuliko Habeck. Wapinzani wake wanamulika ukosefu wake katika uzoefu wa uongozi au uwaziri na makosa ya mara kwa mara katika mahojiano.