Nani wakulaumiwa vifo vya Mahujaji huko Makka?
24 Juni 2024Mamia ya mahujaji wamekufa nchini Saudi Arabia wakati wa kuhiji yumkini kutokana na joto kali. Picha za kushtusha zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii zinazoonesha watu kandoni mwa barabara na za watu waliozirai kwenye viti vya magurudumu. Baadhi ya maiti pia zilionekana kwenye picha hizo.
Habari juu ya vifo vya watu hao, zimethibitishwa baada ya kumalizika kwa shughuli za Hijja. Baadhi wamekufa kutokana na hali ya joto kali na wengine kutokana na ukosefu wa maji au makaazi ya muda.
Soma Pia:Mamia ya mahujjaji wafa Makka kwa joto kali
Joto katika mji wa Makka lilifikia nyuzi joto 51.8 wakati wa shuhguli za kuhiji, wiki iliyopita.Waislamu wapatao milioni 1.8 kutoka duniani kote walitarajiwa kwenda kwenye mji huo kwa ajili ya Hijja.
Wizara ya Afya ya Saudi Arabia inasemaje?
Maafisa wa wizara ya afya nchini Saudi Arabia wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba watu wapatao 2,700 walikumbwa na uchofu. Na kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari watu zaidi ya 1000 wamekufa.
Mahujaji waliokufa walitoka Misri, Indonesia, Senegal, Jordan, Iraq,Iran, India na Tunisia. Serikali za nchi zao zimethibitisha. Idadi kubwa ya waliofariki walitoka Misri. Vilevile idadi ya vifo inaweza kuongezeka kadri juhudi za kuwapata wanaotafutwa zinavyoendelea. Ndugu, jamaa na marafiki bado wanaendelea na juhudi za kuwatafuta mahujaji wasiojulikana walipo.
Soma Pia:Ibada ya Hajj yakamilika na kukaribisha sherehe za Eid Ul Adha
Watu wengi wanaokwenda kuhiji aghalabu ni wazee wanaotaka kutimiza nguzo hiyo kabla ya kufikia mwisho wa maisha yao. Mtu mmoja kutoka Misri amesema Hijja ya mwaka huu ilikuwa ngumu hasa wakati wa kumpiga mawe shetani.
Mhujaji huyo raia wa Misri kutoka mji wa kusini wa Aswan ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia DW kwamba Hija ya mwaka huu haikuwa nzuri na kwamba hakupendezwa na mipango iliyokuwepo.
Mmisri huyo amesema watu walikuwa wanaanguka na kuzirai kutokana na joto kali. Ameeleza kuwa sehemu ya kumpiga mawe shetani katika mlima Arafat ilikuwa mbali na jua lilikuwa kali sana na hivyo kusababisha kiwango cha juu cha joto.
Kumpiga mawe shetani ni sehemu ya ibada ya Hajj inayohusisha mahujaji kurusha mawe kwenye kuta tatu, ikiwa ni mfano wa kumpiga mawe shetani.
Wakati huo huo meneja wa kampuni moja ya utalii nchini Misri amesema joto lilikuwa kali sana nchini Saudi Arabia na kwa bahati mbaya baadhi ya mahujaji hawakufuata maagizo. Hawakujua mambo muhimu waliopaswa kufanya.
Meneja huyo amesema kila mtu alifanya kile alichotaka. Ameeleza kuwa baadhi ya mahujaji hawakulazimika kusimama juu ya mlima Arafat. Mtu angeliweza kuyatimiza yote kwenye sehemu za chini za mlima huo.
Nani wakulaumiwa juu ya vifo vya Mahujaji?
Sasa mijadala mikali imezuka kwenye nchi za watu waliokufa juu ya nani anapaswa kubeba lawama! Baadhi ya familia zinailaumu Saudi Arabia kwa vifo vya mahujaji. Lakini wengine wanawalumu mahujaji waliokwenda Saudi Arabia bila ya kuorodheshwa rasmi.
Soma Pia:Mahujaji milioni mbili waanza safari ya Arafa
Mkurugenzi wa usalama wa umma nchini Saudi Arabia, amesema watu zaidi ya 171,000 waliingia nchini humo kabla ya kuanza kwa shughuli za kuhiji.
Watu ambao hawasajiliwi hawapati huduma zinazostahili, kama vile maji, vipoza joto na mahala pa kukaa. Huenda hizo hasa zikawa ndizo sababu za maafa yaliyotokea.
Pamoja na sababu kadhaa zilizotajwa, jambo moja litaendelea kuwa wazi ni kwamba mabadiliko ya tabia nchi yataendelea kusababisha joto kali nchini Saudi Arabia.
Chanzo: /dw/en/who-or-what-is-responsible-for-hajj-deaths-in-saudi-arabia/a-69428991