1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kuidhinisha kuongeza wanajeshi wake Romania

14 Juni 2016

Jumuiya ya kujihami ya NATO inatarajiwa kuidhinisha rasmi mipango ya kuongeza uwepo wake kijeshi nchini Romania na katika nchi zinazopakana na Bahari ya Baltic, katika kukabiliana na vitendo vya Urusi kuivamia Ukraine.

https://p.dw.com/p/1J6TK
Makao Makuu ya NATO, Brussels
Makao Makuu ya NATO, BrusselsPicha: DW/B. Riegert

Jumuiya ya kujihami ya NATO leo inatarajiwa kuidhinisha rasmi mipango ya kuongeza uwepo wake kijeshi nchini Romania na katika nchi zinazopakana na Bahari ya Baltic, katika kukabiliana na vitendo vya Urusi kuivamia Ukraine.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg amewaambia waandishi wa habari mjini Brussels, kwamba mawaziri wa ulinzi wa jumuiya hiyo wanaokutana mjini humo, watalikubali pendekezo la Romania la kupeleka vikosi vyake nchini humo. Mawaziri hao pia wataidhinisha rasmi mipango ya kupelekwa kwa vikosi vya NATO nchini Estonia, Lithuania, Latvia na Poland.

Stoltenberg amesema watachukua maamuzi ya kuongeza uwepo wa wanajeshi wake katika ukanda wa kusini-mashariki katika mfumo wa brigedi ya kimataifa iliyopo Romania. Amesema kikosi hicho kitaratibu na kuwezesha shughuli za NATO katika ukanda huo hasa zile zinazohusiana na mazoezi ya kijeshi na pia kuhakikisha hatua zinachukuliwa. Hata hivyo, Stoltenberg amesema hawakusudii kufanya mapambano yoyote na Urusi.

''Tunapenda kufikisha ujumbe mzito sana kwamba hatutaki Vita vingine Baridi na tutaendelea kujitahidi kuujenga na kuuendeleza uhusiano wetu na Urusi. Na hasa wakati kuna mvutano mkubwa kama sasa, nadhani ni muhimu tuendelee kuweka wazi milango ya kufanyika mazungumzo ya kisiasa, lakini pia mawasiliano ya kijeshi, kwa sababu tunapaswa kuepuka matukio na ajali kwa mfano tukio la kudunguliwa ndege ya kivita ya Urusi, kulikofanywa na Uturuki,'' amesema Stoltenberg.

Katibu huyo mkuu wa NATO hajatoa maelezo zaidi ni jinsi gani wanajeshi hao watapelekwa Romania, ingawa duru za kidiplomasia zinaeleza kuwa vikosi vinne katika mataifa ya Baltic na Poland vinakusudiwa kuwa na kati ya wanajeshi 2,500 na 3,000.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO, Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Urusi inapinga mipango ya NATO

Urusi imepinga vikali mipango ya NATO kuimarisha uwepo wake wa kijeshi karibu na mipaka ya nchi hiyo na imesema hatua hiyo inaonekana kama kuutishia usalama wa nchi hiyo. Mwezi uliopita, NATO ilifungua kituo cha mfumo wa kujikinga na makombora nchini Romania, hali iliyozusha hasira kwa Urusi, hadi kutoa vitisho kwamba itachukua hatua.

Awali, Waziri Mkuu wa Romania, Dacian Ciolos alitoa wito wa kuongezwa uwepo wa NATO katika Bahari Nyeusi, inayopakana na nchi wanachama wa NATO ambazo ni Bulgaria, Romania na Uturuki, lakini pia Urusi, Georgia na Ukraine.

Viongozi wa NATO wanatarajia kuidhinisha rasmi kuimarishwa kwa mipango ya jumuiya hiyo, ikiwemo kupelekwa kwa vikosi hivyo, katika mkutano wao wa kilele utakaofanyika Poland, kuanzia Julai 8 hadi 9.

NATO imekuwa ikijaribu kujiimarisha zaidi tangu ulipozuka mzozo wa Ukraine na hatua ya Urusi kuivamia Ukraine na kulitwaa jimbo la Crimea mwaka 2014, hali iliyosababisha kuongeza uwepo wa majeshi yake katika mataifa wanachama ambayo yaliwahi kutawaliwa na Urusi kwa lengo la kuwahakikishia kwamba hayatoachwa bila ya msaada.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTR,AFP,DPA,AP
Mhariri:Iddi Ssessanga