1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaadhimisha miaka 70 ikiwa kwenye mizozo

3 Desemba 2019

Wakati mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO yakikutana London kwa mkutano wa kilele unaoadhimisha pia miaka 70 ya ushirika huo mkubwa kabisa wa kijeshi ulimwenguni, tafauti za wazi zinajidhihirisha baina yao.

https://p.dw.com/p/3U9er
NATO-Gipfel in Großbritannien |  NATO-Generalsekretär Stoltenberg und US-Präsident Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele, Rais Trump amewalaumu washirika wa Ulaya, hasa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kauli yake kwamba jumuiya ya NATO iko mahututi, akisema ni kauli chafu dhidi ya muungano huo wa kijeshi; na pia akiikosoa Ujerumani kwa kutumia kiwango kidogo sana cha fedha kwenye masuala ya ulinzi. 

Kwenye mazungumzo yake na waandishi wa habari akiwa na Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, siku ya Jumanne (Novemba 3), Trump alielekeza pia mashambulizi yake dhidi ya ukosoaji wake Uturuki ndani ya jumuiya hiyo, mwanachama ambaye kwa siku za karibuni amekuwa na uhusiano wa karibu na Urusi, hasimu mkubwa wa NATO.

Kwa mujibu wa Trump, Uturuki ni mshirika muhimu sana wa Marekani kwenye vita dhidi ya ugaidi nchini Syria, hasa kufuatia kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu, Abu Bakr Al-Baghdadi.

"Wiki tatu zilizopita tulipompata Al-Baghdadi, Uturuki ilitusaidia sana. Tulipitia maeneo ambayo yanadhibitiwa na  jeshi la Uturuki. Tuliwaambia tunakuja na walitusaidia sana ingawa hatukuwaambia tunakwenda kufanya nini na tunakwenda wapi. Uturuki ilikuwa na ukarimu na ya msaada mkubwa na hilo ni muhimu," alisema.

Mzozo wa NATO na Uturuki

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki Picha: picture alliance/AA/M. Aktas

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa NATO, kuhusiana na ikiwa jumuiya hiyo inaweza kufikia mardihiano na Uturuki ambayo kwa sasa imeagiza mitambo ya kijeshi kutoka Urusi, Stoltenberg alikubaliana na Trump juu ya umuhimu wa Uturuki kwa NATO, ingawa hakuweza kuhakikisha moja kwa moja kuwa pande hizo mbili zitafikia makubaliano.

"Washirika wengi wameeleeza wasiwasi wao juu ya operesheni ya Uturuki kaskazini mashariki mwa Syria lakini baada ya makubaliano kati ya Marekani na Uturuki, baada ya Makamu wa Rais Mike Pence kwenda Ankara, tumeona kwamba Uturuki imeanzisha operesheni zake na mumeona mashambulizi yamepungua sana na sasa lazima tujaribu kusaka suluhisho la Syria," alisema.

Katika kile kinachoashiria kama ni kiwango cha juu ya suintafahamu ndani ya NATO, Trump ameendelea kuwataka washirika wa Ulaya kulipia zaidi masuala ya ulinzi na kuridhia masharti ya kibiashara ya Marekani, huku akitishia vikwazo vipya vya ushuru kwa bidhaa za Ulaya. 

Hata hivyo, Ufaransa na Muungano wa Ulaya zimesema kwa pamoja kwamba ziko tayari kulipiza kisasi endapo Trump atatimiza azma yake ya kuweka ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa za mvinyo, mikoba na bidhaa nyengine zenye thamani ya dola bilioni 2.4 kutoka Ufaransa.

Reuters