NATO yaikingia kifua Ukraine
5 Septemba 2014Poroshenko analiona suala la kusitisha mapigano kuwa muhimu, iwapo Urusi itakubaliana na hatua za kuleta amani. Sekione Kitojo na taarifa zaidi.
Baada ya kikao chao cha kwanza cha mkutano wa NATO mjini Newport , Wales nchini Uingereza suala hilo pia lilijadiliwa iwapo kutapatikana makubaliano. Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen , amedokeza kwamba , matamshi kama hayo yamekwishasikika mara nyingi kutoka Urusi.
Kitu muhimu ni vitendo , amesema Rasmussen akitupia jicho mapambano yanayoonekana hivi sasa mashariki mwa Ukraine. NATO inaishutumu moja kwa moja Urusi, kwa kupeleka maelfu ya wanajeshi wake ndani ya Ukraine kwa nia ya kuwasaidia wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi.
NATO yaikingia kifua Ukraine
Mkutano wa NATO mjini Newport hata hivyo umetoa tamko la wazi kumpa msaada rais wa Ukraine Petro Poroshenko , hata kama ni kwa maneno tu. Kujiingiza kijeshi kwa NATO katika mzozo huo hata hivyo hakuonekani kuwa kunawezekana.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel , alikutana na Petro Poroshenko baada ya kikao hicho na mazungumzo kadhaa pembezoni mwa mkutano huo hayaonekani kutoa matumaini. Wakati wote kumekuwa na mahusiano ya karibu kati ya rais Poroshenko na rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema kansela Merkel.
Iwapo maneno yatafuatiwa na vitendo , kesho ama katika siku zijazo ,hilo litasubiri kufahamika. Kwa hali yoyote iwayo nimeweza kuona matakwa ya rais wa Ukraine, kwamba mchakato wa kisiasa wa kuleta suluhisho unafanyika.
Nimesema kila mara , hakuna suluhisho la kijeshi katika mzozo huu.
NATO amesema kansela Merkel , pamoja na viongozi wengine wa serikali , itasaidia kuijenga upya Ukraine, kisiasa pamoja na kijeshi kwa pamoja na kutoa elimu.
"Tutaisaidia Ukraine na kuonesha mshikamano. Tuko tayari , pia kuweka vikwazo zaidi dhidi ya Urusi iwapo masharti yetu ya kisiasa hayatatimizwa, ameongeza Merkel.
Rais Petro Poroshenko ameishukuru NATO kwa ushirikiano wa muda mrefu kwa kulipa mafunzo jeshi la Ukraine na kusema kuwa baadhi ya mataifa wanachama wa NATO wanataka kulipatia jeshi la nchi hiyo ambalo halina silaha za kutosha , silaha zaidi.
Poroshenko amesema anaweza kuamuru usitishaji mapigano leo iwapo mkutano mjini Minsk utaleta mafanikio.
Leo Ijumaa(05.09.2014) NATO inataka kutoa ushauri vipi mataifa wanachama katika Ulaya mashariki wanaweza kujilinda dhidi ya kitisho kinacholetwa na Urusi. Kutakuwa na uimarishaji wa jeshi litakalochukua hatua kwa haraka na kuliimarisha jeshi hilo katika mataifa ya Baltic.
Mwandishi: Riegert, Bernd /ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Gakuba Daniel