1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yakosoa hatua za Uturuki Syria, lakini hakuna adhabu

24 Oktoba 2019

Mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami NATO, wanakutana Brussels, kuandaa mkutano wa kilele wa wakuu wa mataifa hayo mwezi Desemba, lakini ajenda yao huenda ikagubikwa na operesheni ya Uturuki nchini Syria.

https://p.dw.com/p/3Rrlj
Belgien Brüssel | NATO Generalsekretär Jens Stoltenberg
Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Wiki mbili zilizopita, Uturuki, ambayo ni mwanachama wa NATO ilianzisha operesheni ya kijeshi kaskazini-mashariki mwa Syria kupambana dhidi ya kundi la wapiganaji wa Kikurdi la YPG, ambalo serikali mjini Ankara inalichukulia kuwa kundi la kigaidi lenye mafungamano na kundi la chama cha wafanyakazi wa Kikurdi PKK. Kundi la PKK limeorodheshwa na Uturuki, Umoja wa Ulaya na Marekani kama kundi la kigaidi.

Uvamizi huo, ambao umesimamishwa na mapatano ya kusitisha uhasama, ulikosolewa vikali na washirika wengi wa NATO, kutokana na wasiwasi kwamba ungedhoofisha utulivu wa kikanda na kurejesha nyuma mafanikio yaliopatikana dhidi ya wapiganaji wa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu. Umechochea pia wasiwasi miongoni mwa washirika wengi wa NATO kuhusu mwelekeo wa Uturuki.

Türkei Militärkonvoi an der Grenze zu Syrien
Operesheni ya Uturuki dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria imekosolewa vikali na wanachama wengine wa NATO.Picha: picture-alliance/AP/DHA/Kirikhan/M. Kocacik

"Katika masuala kadhaa tunawaona wanaijongelea zaidi Urusi kuliko mataifa ya Magharibi. Na nadhani hilo ni jambo la kusikitisha. Na nadhani sote tunahitaji kushirikiana ili kuimarisha ushirika wetu na Uturuki, na kuhakikisha wanarudi kuwa mshirika imara anaetegemea, mwenye kuwajibika kama walivyokuwa huko nyuma", alisema waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper.

Wasiwasi wa NATO kuhusu Uturuki

Ankara imewakasirisha washirika wake kwa hatua yake ya kununua mfumo wa ulinzi wa angani wa S400 kutoka Urusi, huku ukandamizaji dhidi ya uhuru wa kiraia ulifuatia jaribio la mapindizi lililoshindwa mwaka 2016, ukitazamwa pia kwa wasiwasi katika miji mikuu mingine. Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amefanya juhudi kubwa kubainisha kuwa Uturuki ni mwanachama muhimu wa kimkakati mwenye maslahi halali ya kiusalama.

Katika mkutano huo, waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulus Akar alitazamiwa kuwaarifu wenzake wa NATO juu ya maendeleo yaliopo, huku waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer, akipanga kuwasilisha pendekezo la kuundwa kwa ukanda salama unaosimamiwa na jumuiya ya kimataifa kaskazini mwa Syria.

Annegret Kramp-Karrenbauer im Interview zu Sicherheitszone in Syrien
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer anataka kuundwe ukanda salama unaosimamiwa na jumuiya ya kimataifa nchini Syria.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Wazo lake linajadiliwa vikali mjini Berlin, ambako bado linasubiri kuidhinishwa na serikali na limekosa msisimko kutoka kwa mataifa washirika. Waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper, amekaribisha wazo hilo, na kusema anaunga mkono kisiasa, wazo la mataifa ya Ulaya kujitokeza kuimarisha usalama, lakini akasema Marekani haitochangia wanajeshi wa ardhini.

Katika mazungumzo yao mjini Brussels, mawaziri hao pia walitazamiwa kujadili namna ya kujiandaa na vitisho mchanganyiko - ikiwemo usalama wa mfumo wa mawasiliano wa 5G - hatua zilizopigwa katika kuimarisha uwezo wa uitikiaji wa haraka, na matukio ya nchini Afghanistan.

Chanzo: Mashirika