1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yasema itasimama na Uturuki katika suala la Syria

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
28 Februari 2020

Washirika wa jumuiya ya kijeshi ya NATO wamelaani mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi na kusabaisha vifo vya askari 33 wa Uturuki katika mkoa wa Idlib.

https://p.dw.com/p/3Yber
Syrien Türkei Kämpfer
Picha: Getty Images/O. Kadour

Jumuiya ya kimataifa imeonyesha hofu ya kuongezeka kwa mashambulio ya vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi katika mkoa wa Idlib, ambapo Rais Bashar al-Assad anaendesha kampeni ya kuwaondoa waasi kutoka kwenye jimbo hilo la mwisho lililo chini ya waasi.

Washirika wa NATO wamelaani mashambulio hayo yaliyofanywa na vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi na wameeleza kamba wanashikamana na mshirika wao Uturuki, ambayo ni ya pili kwa kuwa na kikosi kikubwa katika muungano huo wa kijeshi.

Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, ametoa wito kwa Urusi na Syria kusimamisha mara moja kampeni yao ya kuukomboa mkoa wa Idlib.Stoltenberg amesema hali hii hatari ni lazima iepukwe, na ametoa wito wa kurejea mara moja kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano yya 2018 ili kuepusha kuongezea hali mbaya ya kibinadamu katika mkoa huo.

Katibu Mkuu wa jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Marais wa Urusi na Uturuki walizungumza kwa njia ya siku ya Ijumaa baada ya askari 33 wa Uturuki kuuawa kwenye shambulio la ndege katika jimbo la Idlib. Uturuki moja kwa moja imeilaumu Syria. Wakati Urusi ikikanusha kuhusika na shambulio pande zote zimeshauriwa kuheshimu sheria za kimataifa. 

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wamesisitiza kwenye mazungumzo yao kwamba wanajeshi wao ni lazima wawe na ushirikiano katika jimbo hilo la Idlib ambalo ni ngome ya mwisho inayodhibitiwa na waasi nchini Syria na pia wamekubaliana kukutana haraka iwezekanavyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema ingekuwa vyema kama wanajeshi watafuata makubaliano yaliyopo ambayo ni pamoja na mawasiliano juu ya eneo halisi wanapokuwa wanajeshi wa Uturuki ili kuepuka majanga.

Wakati huo huo Uturuki imeonya kuwa itafungua milango kwa wakimbizi wanaotaka kuingia Ulaya, hatua ambayo inaweza kuleta athari kubwa kwa jirani zake wa magharibi na imeifanya Ugiriki kuongeza  doria katika mpaka wake.

Vyanzo: DPA/AP