1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yataka ushirikano na China kuhusu Afghanistan

Saleh Mwanamilongo
28 Septemba 2021

Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO ametaka ushirikiano wa karibu na China kushughulikia serikali mpya ya Afghanistan, huku Taliban ikionywa vikali.

https://p.dw.com/p/40yGo
Symbolbild Beziehungen China - NATO
Picha: edna/imago images

Kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya video na waziri wa China wa mambo ya nje Wang Yi, katibu mkuu wa jumuiya ya NATO Jens Stolenberg ameomba kuweko na mtazamo wa pamoja baina ya China na Nato kuhusu Afghanistan.

Taarifa iliotolewa na jumuiya ya kujihami ya NATO kufuatia mkutano huo,inasema Stolenberg alisisitizia umuhimu wa hatua iliyoratibiwa kwenye ngazi ya kimataifa ilikuishinikiza Taliban kuheshimu ahadi zake za kupambana na ugaidi na kuheshimu haki za binadamu.

Kundi la Taliban lenye msimamo mkali wa Kiislamu lilichukua udhibiti wa Afghanistan baada ya kuondoka kwa ujumbe wa kijeshi wa miongo miwili wa jumuiya ya NATO,ambao lengo kuu lilikuwa haswa kuzuwia Taliban kurejea madarakani.

Jumuiya ya NATO inahofu kwamba China huenda ikajaribu kuchukuwa fursa hiyo kuendesha sera yake ambayo itakuwa na matokeo mabaya kwa watu wa Afghanistan.

Soma pia:Mataifa makubwa yataka serikali ya wote Afghanistan 

Athari za kuporomoka kwa uchumi

NRC imetoa wito kwa wafadhili kutoa michango ya kuisaidia Afghanistan
NRC imetoa wito kwa wafadhili kutoa michango ya kuisaidia AfghanistanPicha: AP

 Nchini Afghanistan kwenyewe Baraza la Wakimbizi la Norway, NRC ambalo ni shirika la msaada wa kiutu, limetahadharisha kuhusu kuporomoka kwa uchumi wa Afghanistan, hali itakayozidisha ugumu wa maisha katika taifa hilo linaloandamwa pia na upungufu mkubwa wa chakula.

Katibu Mkuu wa shirika la NRC, Jan Egeland amesema familia nyingi zinamahitaji ya chakula.

"Idadi kubwa ya watu wa nchi hii, takriban nusu ya idadi jumla, maana yake karibu milioni 20 wanahitaji msaada wa dharura mnamo msimu wa baridi unakaribia. Kati ya idadi ya watu milioni 40. Hawa ni sawa na milioni 40 ambazo nchi za NATO ziliwatelekeza wakati zilipoondoka'' alisema Egeland.

Taarifa ya shirika hilo imesema tangu mwezi Januari zaidi ya Waafghani laki sita wamepoteza makaazi na kufanya idadi ya watu wasio na mahali pa kuishi nchini Afghanistan kufikia milioni 3.5.

Soma pia:Taliban wataka kuzungumza katika baraza la Umoja wa Mataifa 

Viongozi wa Pentagon kuhojiwa

Maafisa wa Pentagon kuhojiwa kuhusu bomu la kujitoa muhanga lilolipuka mjini Kabul
Maafisa wa Pentagon kuhojiwa kuhusu bomu la kujitoa muhanga lilolipuka mjini Kabul Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Wakati huohuo viongozi wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon watakabiliwa na maswali makali bungeni, kuhusu machafuko yaliyotokea wakati nchi hiyo ikiondoa wanajeshi wake Afghanistan.

Wanachama wa chama cha Republican hasa ndiyo wamekuwa wakimshambulia zaidi Rais Joe Biden kwa kuwaondosha wanajeshi hao Afghansitan wakidai kuwa hatua hiyo imehataraisha usalama wa Marekani.

Aidha wanataka maelezo zaidi juu ya bomu la kujitoa muhanga lilolipuka mjini Kabul na kusababisha vifo vya Wamarekani 13, katika siku za mwisho za mchakato wa kuwaondoa wanajeshi Afghanistan.