1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yatimiza miaka 75 tangu kuasisiwa kwake

4 Aprili 2024

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameihimiza Marekani kuendelea kuwa pamoja na Ulaya, wakati Jumuiya hiyo ya kijeshi ya nchi za Magharibi ikiadhimisha miaka 75 tangu kuundwa kwake huku ikikabiliwa na changamoto kubwa.

https://p.dw.com/p/4eQBY
NATO yafikisha miaka 75 tangu ilipoasisiwa
Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Jumuiya ya kujihami NATO wakikata keki na kusherehekea maadhimisho ya miaka 75 tangu kuunda Jumuiya hiyo Aprili 4, 1949Picha: Kenzo Tribouillard/AFP/Getty Images

Akizungumza katika hotuba ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuasisiwa kwa Jumuiya hiyo ya kujihami NATO, Jens Stoltenberg  amesema Ulaya na Marekani zinahitajiana kwaajili ya usalama wao. Amesema Ulaya inaihitaji Marekani na Amerika ya kaskazini inaihitaji Ulaya kwa usalama huo. Stoltenberg amesema washirika wa Ulaya  wanatoa kiwango cha juu kabisa cha jeshi, mitandao mipana ya kijasusi na fursa ya kidiplomasia. Amesema kupitia NATO Marekani ina marafiki na washirika wengi zaidi kuliko taifa lolote lililo na nguvu duniani.

Wakati Jumuiya hiyo ikiadhimisha miaka hiyo 75 ya uwepo wake, nchi wanachama 32 wa Jumuiya hiyo walikubaliana kuanza kupanga jukumu kubwa katika kuratibu msaada wa kijeshi kwa Ukraine, kuisaidia kupambana na uvamizi wa Urusi ulioanza mwezi Februari mwaka 2022, uvamizi uliosababisha mgogoro mkubwa zaidi kuwahi kuonekana barani Ulaya, tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.

Mawaziri kuadhimisha miaka 75 ya kuundwa kwa Jumuiya ya NATO

Stoltenberg aliwataka wanachama kuonyesha umoja wao kwa Ukraine wakati taifa hilo la zamani la Kisovieti likisubiri msaada wa dola bilioni 60 ambao umeshindwa kupitishwa na bunge la Marekani.

Viongozi wa Ulaya walio wengi katika Jumuiya ya NATO wana wasiwasi sio tu kuhusu siku za usoni za Jumuiya hiyo iwapo rais wa zamani wa Marekani Donald Trump atamshinda mpinzani wake rais wa sasa wa Marekani Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu, lakini pia juu ya msaada wa fedha kwa Ukraine uliokwama kuidhinishwa Marekani kufuatia wanachama wa Republican kutaka hakikisho pana la usalama kabla ya kupitisha muswada huo.

Masaada zaidi wa kifedha watolewa kwa Ukraine kwa miaka mitano ijayo

Dmytro Kuleba
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ukraine Dmytro KulebaPicha: John Macdougall/AP/picture alliance

Hata hivyo Stoltenberg alipendekeza msaada wa yuro bilioni 100 wa kijeshi kwa Ukraine kwa muda wa miaka mitano. Hii leo mawaziri wa mambo ya nje wa NATO watakutana na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, aliyesema atawahimiza kuipa Ukraine mifumo ya kujilinda na makombora ili kujilinda na makombora yanayovurumishwa nchini humo kutoka Urusi.

Mawaziri wa mambo ya nje wa NATO wajadili mfuko wa yuro bilioni 100 kwa Ukraine

NATO ilianzishwa Aprili 4 mwaka 1949 ikiwa na wanachama 12 kutoka Amerika ya Kaskazini na Ulaya na iliundwa kwa hofu kwamba muungano wa kisovieti ulitoa kitisho kwa mataifa ya Ulaya. Nia yake ni kulinda mataifa wanachama kwa maana ya kwamba taifa moja mwanachama likishambuliwa basi shambulizi hilo moja kwa moja linachukuliwa kama shambulizi kwa mataifa yote na kutoa ulinzi wa kijeshi wa Marekani kwa nchi za Ulaya Magharibi. (SW): NATO yatimiza mi...

Miaka 75 baadae NATO imetanuka zaidi na kuwa na wanachama 32 na kuchukuwa jukumu kubwa katika masuala ya dunia baada ya Urusi kuishambulia Ukraine hatua iliyosababisha serikali za Ulaya kuiona tena Moscow kama kitisho kikubwa cha usalama.

afp/ap/reuters