1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi kama ngome au nchi huru?

Maja Dreyer12 Oktoba 2006

Nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani zilikubaliana juu takwimu zinazomhusu msafiri wa Ulaya anayekwenda Marekani. Kulingana na maafikiano haya wizara ya ulinzi wa nchi ya Marekani itapata takwimu hizi kutoka idara moja ya Umoja wa Ulaya. Halafu, wizara hiyo inaweza kutumia takwimu hizo katika idara zote zinazoshughulikia vita dhidi ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/CHmO
Takwimu nyingi za abiria zitapelekwa Marekani
Takwimu nyingi za abiria zitapelekwa MarekaniPicha: picture-alliance / dpa

Ikiwa raia wa Umoja wa Ulaya anasafiri kwenda Marekani, tayari mzigo mkubwa wa takwimu umefika Marekani kabla ya yeye kuwasili. Kila shirika la ndege linatakiwa kupeleka takwimu nyingi kwa wizara ya ulinzi ya Marekani. Mark Rotenberg wa shirika la kulinda takwimu za kibinaasi anaelezea matokeo ya makubaliano haya: “Kuhusiana na ratiba ya safari, basi serikali ya Marekani itakuwa na habari zaidi kuliko serikali ya msafiri mwenyewe, kwani hakuna hata nchi moja ya Umoja wa Ulaya inayokusanya takwimu hizo.”

Takwimu zinazopelekwa Marekani zinahusu kila hatua ya maandalizi ya safari, yaani jina, anwani, nambari za simu, nambari za akauti za benki, anwani za barua pepe, siku ya kupanga safari, ratibu ya safari, wasafiri wengine wa abiria huyu, idadi ya masanduku yake au kwa mfano pia ikiwa ana hitaji chakula cha aina fulani kama Waislamu ambao hawali nguruwe.

Kwa jumla aina 34 za takwimu zinaweza kupelekwa Marekani. Juu ya hayo, takwimu hizo zinaweza kuhifadhiwa kwa muda wa miaka mitatu na nusu – jambo ambalo linakosolewa na wale wanaotaka kuwalinda watu wa kawaida kama Mark Rotenberg. Anasema: “Ikiwa Marekani kweli inataka kujilinda dhidi ya mashambulio ya kigaidi kutoka angani – sawa! Lakini ikiwa ni hivyo wanaweza kufuta takwimu baada ya abiria kushuka kwenye ndege, kwani mashambulio hayakutokea. Hata hivyo, Marekani inasisitiza kuwa inataka takwimu hizo – haya yananionyesha kuwa ina sababu nyingine ya kukusanya habari hizo zote.”

Makubaliano hayo kuhusu takwimu zinazomhusu msafiri yatakamilika mwezi wa Julai, mwakani. Kwa hivyo Umoja wa Ulaya utakuwa na uwezo mpya wa kusimamisha juhudi za Marekani kukusanya takwimu za kibinafsi za raia na wageni wake. Wakosoaji kama Bw. Rotenberg wanapinga vikali mwenendo huo katika nchi ya kidemokrasi kukusanya habari za kibinafsi zinazowahusu raia wake. Ikiwa Marekani inaendelea hivyo, basi itakuwa sawa na ngome ambaye inawazuia wengine badala ya kuwa ni nchi huru, haya ni maneno ya wakosoaji.