1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi tano zajiunga na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa

18 Oktoba 2013

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limezichagua nchi tano kuwa wanachama wapya wasiokuwa na viti vya kudumu wa baraza la usalama la umoja huo katika uchaguzi ambao haukuwa na ushindani mkali kama siku za nyuma

https://p.dw.com/p/1A1wh
Picha: Reuters

Nchi tano mpya kujiunga na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kama wanachama wa muda ni Lithuania, Nigeria, Chile, Chad na Saudi Arabia ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari mosi mwakani hadi mwishoni mwa mwaka 2015.

Katika duru ya kwanza ya upigaji kura katika baraza hilo kuu la wanachama 193, Lithuania ilipata kura nyingi zaidi 187 ikufuatiwa na Nigerai na Chile zilizopata kura 186, Chad kura 184 na Saudi Arabia kura 176.

Hakukuwa na ushindani kipindi hiki

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi mingi hakukuwa na upinzani katika shughuli hiyo ya kuzichagua nchi hizo tano ambazo zitajiunga na baraza hilo lenye umuhimu mkubwa kwani linazipa nchi hizo usemi mkubwa katika masuala ya kimataifa kuhusu amani na usalama kwa mizozo kama ya Syria, Iran na Korea Kaskazini, pamoja na operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki MoonPicha: picture alliance/abaca

Afrika inawakilishwa na Chad na Nigeria ambao watachukua mahala pa Morocco na Togo. Saudi Arabia itaiwakilisha kanda ya Asia na Pacifiki, nafasi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Pakistan. Chile itachukua mahala pa Guatemala kuiwakilisha kanda ya Amerika ya kusini na mashariki mwa Ulaya kutawakilishwa na Lithuania, kiti kilichokuwa kikikaliwa na Azerbaijan.

Chad, Saudi Arabia na Lithuania hazijawahi kuhudumu katika baraza hilo la usalama lenye wanachama 15 ilhali Nigeria na Chile zimeshahudumu kama wanachama wasiokuwa na viti vya kudumu mara nne kipindi cha nyuma. Nchi wanachama wa kudumu wa baraza hilo ni Urusi, China, Ungereza, Marekani na Ufaransa.

Nchi tatu zatiliwa shaka

Licha ya kuwa nchi hizo tano zilichaguliwa kwa karibu asilimia 100 ya kura, kuchaguliwa kwa Chad, Nigeria na Saudi Arabia tayari kumezua shaka kutoka kwa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch.

Mkurugenzi wa shirika hilo katika Umoja wa Mataifa, Philippe Bolopion, amezitaka nchi hizo kujirekebisha kutokana na rekodi yao mbovu ya haki za binaadamu kwani sasa wamejiunga na baraza lenye hadhi kuu ulimwenguni.

Chad imetakiwa kushughulikia na kukomesha mara moja kutumika kwa watoto kama wapiganaji, jambo ambalo limeiweka nchi hiyo katika orodha ya fedheha ya Umoja wa Mataifa.

Makao makuu ya umoja wa Mataifa mjini Newyork
Makao makuu ya umoja wa Mataifa mjini NewyorkPicha: picture-alliance/dpa

Saudi Arabia inapaswa kusitisha ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa haki za binaadamu na kuheshimu kikamilifu haki za wanawake. Wanawake nchini humo hawaruhusiwi kupiga kura, kuendesha magari wala kusafiri bila idhini ya mume au jamaa wa kiume.

Na Nigeria inapaswa kumaliza ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanywa na maafisa wa usalama na kuwalinda zaidi raia wake wa kaskazini mwa nchi hiyo dhidi ya mashambulizi ya kundi la Boko Haram.

Nchi hizo tatu hazikuzungumzia shutuma hizo katika hotuba zao za kukubali kuhudumu katika baraza hilo la usalama. Waziri wa mambo ya nje wa Chad, Moussa Faki, amesema kuchaguliwa kwa nchi yake kunaonyesha kutambuliwa kwa juhudi za nchi hiyo kuleta amani na usalama Afrika.

Balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa, Abdallah Al Mouallimi, amesema kuchaguliwa kwa nchi yake ni kutokana na sera zake za muda mrefu za kuunga mkono misimamo ya wastani na kutatua mizozo kwa njia za amani.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Nigeria, Viola Onwuliri, amesema nchi yake itaangazia kuzuia mizozo, diplomasia, upatanishi, kukabiliana na ugaidi na kulindwa kwa kila mtu. Waziri aidha amesema watatumia wadhifa huo kuzungumza kwa niaba ya Afrika kwani masuala ya bara hilo ndiyo yanayotawala ajenda za baraza hilo la usalama kwa sasa.

Mwandishi:Caro Robi/ap/dpa

Mhariri: Josephat Charo