Nchi za G77 na China zinakutana nchini Cuba leo
15 Septemba 2023Kundi la nchi 77 zinazoendelea na zinazoinukia la G77 na China, zimekusanyika nchini Cuba leo katika mkutano unaotafuta kukuza utaratibu mpya wa kiuchumi ulimwenguni, katikati mwa ongezeko la migawanyiko.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye aliwasili kisiwani humo jana Alhamisi, ataungana na wakuu wa nchi na serikali kutoka Afrika, Asia na Amerika Kusini katika mkutano wa siku mbili unaofanyika mjini Havana.
Kundi la G77 lilianzishwa mwaka 1964 na mataifa 77 kutoka nchi zinazoendelea ili kueleza na kukuza maslahi yao ya pamoja ya kiuchumi na kuongeza uwezo wa mazungumzo ya pamoja. China sio mwanachama kamili wa kundi hilo. Ijapokuwa wanachama wa kundi hilo sasa wameongezeka na kufikia 134, bado kundi hilo limesalia na jina lake la G77 ili kuzingatia historia yake.