Marekani yapinga muswada wa UN wa kusitisha mapigano Gaza
9 Desemba 2023Azimio hilo la Umoja wa Mataifa liliungwa mkono na wanachama 13 kati ya 15 wa Baraza hilo. Uingereza ambayo ni mwanachama mwingine wa kudumu wa Baraza la Usalama haikupiga kura.
Naibu Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Robert Wood amelikosoa baraza hilo baada ya kura hiyo, akisema limeshindwa kulilaani shambulizi la wanamgambo wa Hamas nchini Israel pamoja na kutambua haki ya Israel ya kujilinda. Ameongeza kuwa kusitisha mapigano kutatoa mwanya kwa Hamas kuendelea kulitawala eneo la Gaza na kufanya mashambulizi mengine ya kigaidi.
Wood, amesema, azimio hilo pia halikuzingatia uhalisia wa mambo na wala haliwezi kubadilisha chochote huko Gaza.
Marekani inalipinga azimio hili licha ya maonyo ya shirika la kimataifa linaloshughulikia afya, WHO kwamba hali inazidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza. Msemaji wa Shirika hilo Christian Lindmeier amesema watu katika eneo hilo sasa wanakata milingoti ya nyaya za simu na kuwashia moto wa kuota ili angalau kujikinga na baridi na pengine kupikia, pale wanapokuwa na chochote cha kupika.
Guterres aonya dhidi ya 'adhabu ya pamoja' kwa Wapalestina
Kabla ya kikao hicho cha dharura, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ukatili unaofanywa na wanamgambo wa Hamas usitumike kuhalalisha adhabu ya pamoja kwa Wapalestina.
Guterres amesema hayo huku akitoa wito wa kuachiliwa mara moja mateka 130 ambao bado wanazuiwa na Hamas, tena bila ya masharti yoyote.
Aidha, amerudia tena kauli yake kwamba hakuna mahali salama katika Ukanda wa Gaza na raia wameshiwa chakula.
IDF: Wanajeshi wawili wajeruhiwa katika jaribio la kuokoa mateka
Nchini Israel, jeshi la taifa hilo, IDF limesema jana Ijumaa kwamba wanajeshi wake wawili walijeruhiwa vibaya baada ya kujaribu kuwaokoa mateka wanaozuiwa Gaza. Limesema katika operesheni hiyo, watekaji wawili pia waliuawa na hakukuwa na mateka yoyote aliyeokolewa.
Hamas, ambao wanaorodhoshwa kama magaidi na Marekani, Ujerumani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine wamesema kwenye taarifa yao kwamba walifanikiwa kulizuia jaribio la Israel la kuwaokoa mateka wa Israel inaowashikilia. Bila ya kuthibitisha, wanamgambo hao wamesema mateka mmoja aliuawa wakati walipokabiliana na wanajeshi wa IDF. Israel haikazungumzia madai hayo.
Umoja wa Ulaya wawaongeza viongozi wa Hamas kwenye orodha ya ugaidi
Huku hayo yakiendelea, Umoja wa Ulaya jana Ijumaa umewaweka makamanda wawili wa Hamas katika orodha ya magaidi, kama sehemu ya kujibu kitisho kinacholetwa na kundi hilo pamoja na mashambulizi yake ya kigaidi nchini Israel, Oktoba 7, 2023. Makamanda hao ni mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas, Mohammed Deif na naibu wake Marwan Issa.
Baraza la Umoja huo limesema, fedha za viongozi hao wawili pamoja na mali nyingine za kifedha katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, zitazuiwa.