1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Magharibi zavutana na Urusi kuhusu mamluki

Josephat Charo
24 Juni 2021

Marekani, Uingereza na Ufaransa zimewatuhumu mamluki wa Urusi kwa kushirikiana bega kwa bega na vikosi vya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kufanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/3vUGQ
Mankeur Ndiaye - Leiters der UNU-Mission in der Zentralafrikanischen Republik
Mankeur Ndiaye, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: SCPI/UN/MINUSCA

Malumbano hayo yametokea katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya mjumbe maalumu wa umoja huo kwa ajili ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mankeur Ndiaye, kuelezea wasiwasi mkubwa kuhusu harakati ya kijeshi inayofanywa na vikosi vya taifa hilo pamoja na vikosi shirika na vingine vya usalama, katika mapambano dhidi ya muungano wa makundi ya waasi yanayomuunga mkono rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Francois Bozize.

Ndiaye ameieleza hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa miongoni mwa hali hatari kabisa duniani, akisema vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na sheria ya kimataifa vinavyodaiwa kufanywa na vikosi vya nchi hiyo na vikosi vingine vinavyoshirikiana navyo, havijafikia vile vilivyofanywa hivi karibuni na kuorodheshwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA.

"Ninabaki kuwa na wasiwasi kuhusu matokeo hasi yanayosababishwa na harakati za kijeshi zinazofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama, na washirika wao, kuyachakaza makundi ya wapiganaji wa chini kwa chini na makundi ya waasi wenye silaha wanaofanya ukiukaji wa haki za binadamu. Hali hii imesababisha hali mbaya ya kibinadamu isiyo mithili huku kukiwa na wimbi jipya la watu kuyakimbia makazi yao wakihitaji msaada wa kiutu."

Mfano mmojawapo alisema ni idadi ya matukio ya unyanyasaji wa ngono katika robo ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa mara tatno zaidi kuliko idadi iliyoripotiwa katika robo ya mwisho ya mwaka uliopita. Ingawa Ndiaye hakuvitaja vikosi washirika na vikosi vingine vinavyopigana bega kwa baga na wanajeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Urusi ina wanajeshi wake nchini humo walioalikwa na serikali.

Urusi yakanusha madai kuhusu mamluki

Hata hivyo naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Anna Evstigneeva, amejibu akisema wakufunzi wa Urusi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamepata mafanikio makubwa wakiimarisha ujuzi wa vikosi vya taifa hilo la Afrika bila kushiriki katika harakati za kijeshi dhidi ya makundi yaliyojihami na silaha. Amesema kuna juhudi za makusudi zenye nia mbaya ya kuwachafua bila ushahidi wowote, hususan katika vyombo vya habari nchini Marekani na Ufaransa, ambavyo hutumia vyanzo visisivyotambulishwa na hii inaonekana zaidi kama kampeni chafu ya kisiasa ya kuichafua Urusi.

Zentralafrika Bangui UN Wahlen
Gari la tume ya MINUSCA likiwa katika doria mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, BanguiPicha: Antonie Rolland/REUTERS

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Richard Mills aligusia ripoti ya katibu mkuu wa umoja huo Antonio Guterres kuhusu ongezeko la asilimia 28 ya matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Mills aidha amesema Marekani ina wasiwasi mkubwa kuhusu kulengwa waislamu, na ongezeko kubwa la udhalilishaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali na washirika wao.

Mills amesema utawala wa rais Joe Biden una mashaka makubwa kwamba Urusi imeshindwa kuwazuia mamluki wake kukwamisha kazi ya MINUSCA na kuwatatiza kila siku wanajeshi kutembea kwa uhuru. Amelaani vikali tukio la Mei 28 ambapo mamluki wa Urusi walimtishia maisha naibu wa mjumbe maalumu wa MINUSCA na ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia utoaji wa misaada ya kibinadamu huko Bang, mji ulio karibu na mpaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad na Cameroon.

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Nicolas De Riviere ameitaja hali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa ya kutisha, akizungumzia mauaji ya kiholela kinyume cha sheria, ubakaji wa magenge, mateso, shule kutekwa na kudhibitiwa na machafuko dhidi ya jamii za waislamu. Balozi huyo amesema baadhi watajaribu kukanusha uwepo wa kampuni ya usalama ya Wagner, ambayo inaungwa mkono na utawala wa Kremlin, iliyotajwa kuhusika pia katika mzozo wa Libya.

Naibu balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa James Roscoe amesema makundi ya wapiganaji yanachochea machafuko na kuyumbisha hali ya usalama kwa masilahi yao.

(ap)