1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kushinikiza kukomesha nishati za visukuku.

1 Septemba 2023

Umoja wa Ulaya unapanga kushinikiza makubaliano ya kukomesha nishati za visukuku. Wazo hilo litatolewa kwenye mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa - COP28 mjini Dubai.

https://p.dw.com/p/4Vr05
Deutschland, Berlin | Petersberger Klimadialog
Picha: Tobias Schwarz/AFP/Getty Images

Wnadiplomasia kutoka nchi 27 wanachama wa Umoja huo wanaandaa rasimu kuhusu msimamo wao huo na ambao watautoa kwenye mkutano wa kilele wa COP28 utakaofanyika mjini Dubai mwezi ujao wa Novemba, ambako karibu nchi 200 zinajaribu kuimarisha juhudi za kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa.

Rasimu hiyo ya Umoja wa Ulaya iliyoonekana na shirika la habari la Reuters imesema mabadiliko kuelekea uchumi unaolinda hali ya hewa yatahitaji mataifa yote kushirikiana katika kuondokana na nishati za kisukuku kwa awamu na kilele chake ni pale matumizi ya nishati hizo yatakapositishwa katika muda wa hivi karibuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock katika mkutano wa kuandaa rasimu ya mkutano wa COP28.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock katika mkutano wa kuandaa rasimu ya mkutano wa COP28.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wanatumai kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa katika mkutano huo wa COP28 lakini wametilia maanani kuwa watakutana na upinzani kutoka kwa nchi ambazo uchumi wake unaotegemea mapato kutokana na mauzo ya mafuta na gesi.

Rasimu hiyo ya Umoja wa Ulaya, ambayo bado inajadiliwa na inaweza kufanyiwa mabadiliko kabla ya kukamilika mwezi Oktoba, inataja kuwa sekta ya nishati inapaswa kuondokana na nishati hizo za visukuku kwa kiwango kikubwa kabla ya mwaka 2050 kwa sababu vyanzo vya nishati visivyo na Hewa Ukaa gharama yake ni nafuu na tayari vinapatikana.

Pendekezo la kukomesha mafuta ya petroli yanayotoa hewa chafu ya ukaa liliungwa mkono na zaidi ya nchi 80 katika mkutano wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa wa mwaka jana lakini Saudi Arabia na mataifa mengine yenye utajiri wa mafuta na gesi yalilipinga pendekezo hilo.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Baadhi ya nchi zinazouza wa mafuta ghafi zinataka kuzingatia kuendeleza teknolojia za kunasa uzalishaji wa Hewa Ukaa badala ya kupunguza matumizi ya mafuta. Hali hiyo ya kupishana katika swala hili inamaanisha mawaziri wa nchi za kundi la G20 hawakuweza kukubaliana njia za kukabiliana na nishati za visukuku katika mkutano wao wa mwezi uliopita.

Ingawa sio lazima kisheria, wazo la mpango wa kimataifa wa kuondokana na nishati za visukuku hatua kwa hatua linalenga kuunda msimamo wenye nguvu utakaoongoza mazungumzo ya hali ya hewa siku zijazo, sera za serikali na uwekezaji kuelekea vyanzo vya nishati na teknolojia ambazo hazisababishi joto kuongezeka joto kwenye sayari.

Chanzo: RTRE