Nchi zinazolima pamba Afrika zaitaka WTO kusaka suluhisho
26 Februari 2024Wito huo ulitolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 13 wa Mawaziri wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) mjini Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Nchi hizo zinazoitwa C4 zinazoijumuisha Benin, Burkina Faso, Mali na Chad, zilitoa wito wa kukomeshwa kwa ruzuku ya pamba kwa nchi kama Marekani, India na China, ambazo zinasema zinaathiri bei ya ndani ya pamba.
Akizungumza kwa niaba ya C4, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Chad, Ahmat Abdelkerim, amewaambia waandishi habari mjini Abu Dhabi kwamba kwa muda wa miaka 20 iliyopita, upotoshaji wa biashara ya pamba umeendelea kuhatarisha maisha ya mamilioni ya wazalishaji wa pamba barani Afrika.
Ivory Coast na C4 ziliwasilisha rasimu ya uamuzi kuhusu pamba kwa WTO kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo katika Umoja wa Falme za Kiarabu unaoanza leo Jumatatu.